Kimataifa

Raia Madagascar kuendelea kuzongwa na umaskini – Ripoti

February 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MASHIRIKA

ANTANANARIVO, MADAGASCAR

BENKI ya Dunia imeonya viwango vya umaskini nchini Madagascar vitaendelea kuongezeka baada ya tathmini ya umaskini kufikia asilimia 75.2 ikilinganishwa na asilimia 72.9 mwaka 2012.

Benki hiyo ilifichua kwamba watu nchini humo waliishi chini ya kiwango cha umaskini wa kitaifa mwaka 2022.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa, kiwango cha umaskini vijijini unaendelea kukua kwa hali ya juu ambayo ni asilimia 79.9 mwaka 2022.

Wakati umaskini mijini umeongezeka kutoka asilimia 42.2 mwaka 2012 hadi asilimia 55.5 mwaka 2022, hasa katika miji ya viwango vya pili.

Pia, ilionyesha viwango vya umaskini vinatofautiana kote Madagascar, huku Androy kusini ikiwa na kiwango cha juu zaidi cha umaskini.

Wakati huo huo, mikoa ya kaskazini ina viwango vya chini vya umaskini kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kama vile utalii na uzalishaji wa vanila.

Kinyume na upande wa Mashariki mwa nchi ambapo eneo la umaskini mkubwa umetokana na vimbunga vya mara kwa mara, ambavyo husababisha uharibifu mkubwa na hasara ya mali miongoni mwa jamii zinazoishi eneo hilo.

Ripoti hiyo ilionyesha ongezeko la umaskini lilichangiwa zaidi na janga la Covid-19, lakini pia bei za juu za vyakula na majanga kama vile kiangazi yanafanya hali kuwa mbaya zaidi.

Pia, kuongezeka kwa idadi ya watu mijini kutafuta fursa za ajira ambazo ni chache zikipatikana katika miji ya kiwango cha pili.

Matatizo chungu nzima yakiwemo uzalishaji mdogo wa sekta ya kilimo na ukosefu wa huduma za msingi katika maeneo ya vijijini, mtaji dhaifu kwa watu, viwango vya juu vya uzazi, uwezekano mkubwa wa kukabiliwa na majanga ya mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa utulivu wa kisiasa na migogoro ya kimataifa, pamoja na ukosefu wa fursa za kiuchumi, vimechangia hali hiyo.

Meneja wa Benki ya Dunia nchini Madagascar Atou Seck alisema kukabiliana na umaskini humo, Madagascar inahitaji mageuzi ya kijasiri ya kukuza uchumi, ambayo yanapaswa kuboresha hali ya biashara, kukuza ushindani, kuwepo kwa mtaji wenye manufaa kwa watu, kuwekeza katika mawasiliano, upatikanaji wa nishati na miundombinu ya kidijitali, pamoja na kuongeza kiwango cha mavuno katika kilimo.

“Kwa kutekeleza hatua hizo, Madagaska inaweza kuweka mazingira ya kuwezesha ambayo yanakuza ukuaji wa sekta binafsi na uzalishaji wa ajira ili kupunguza umaskini. Haya yote, hatimaye yatanufaisha wakazi wote,” alisema Seck.