Habari MsetoSiasa

Muafaka wa Uhuru na Raila wafaa kuwaletea Wakamba maendeleo – Ngilu

December 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA STEPHEN MUTHINI

GAVANA wa Kitui Bi Charity Ngilu amesema kuwa ushirikiano kati ya viongozi wa kisiasa ulioundwa baada ya muafaka Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Bw Raila Odinga unafaa kuleta ushirikishi serikalini na kuimarisha maendeleo ili kuwakomboa wananchi kutoka kwa umaskini.

Gavana huyo aliyehutubu katika Kanisa la Katoliki la St Christopher Kyumbi, Machakos Jumapili alisema kiongozi wa chama cha Wiper Bw Kalozno Musyoka anafaa kumwalika Rais Kenyatta Ukambani ili kutoa mwelekeo wa jinsi muafaka huo utawafaa wakazi wa eneo hilo.

“Ni vizuri kuona taifa hili likiwa na amani lakini tunafaa kuona mengi zaidi kuhakikisha wananchi hawateseki na mambo ambayo muafaka huo hauwezi kusuluhisha,” akasema Bi Ngilu.

Alishangaa jinsi miaka 55 tangu nchi hii ipate uhuru, bado wananchi wamekwama kwa umaskini na ukosefu wa maendeleo.

“Muafaka huu unafaa kutuleta pamoja na kuona jinsi tutatumia rasilimali zetu kimaendeleo na kuwaimarisha vijana wetu katika uzalishaji,” akasema.

Alielezea kuwa vijana wengi walijitokeza katika ziara ya Rais jijini Kisumu wakitarajia kuwa umoja mpya baina ya viongozi wakuu utawaletea manufaa maishani.

Bi Ngilu alisema umoja huo sasa unafaa kutumiwa kutekeleza miradi muhimu Ukambani kama Bwala la Thwake, Jiji la Kiteknolojia la Konza ambayo alisema serikali imekuwa ikijikokota kuitekeleza.

Alisema kuwa wananchi hawawezi kuzidi kusubiri maendeleo kwa miaka mingi huku viongozi wakizidi kutoa ahadi hewa.

“Wakati umefika sasa kupiga darubini ukweli wa mambo. Hatuwezi kuzidi kuwapigia makofi viongozi ambao hawajasaidia lolote kutokomeza umaskini,” akasema huku akikariri maneno ya Rais wa Amerika Donald Trump aliyesema viongozi wa Afrika wamelemewa kuwanasua wananchi wake kutoka kwa changamoto za kiuchumi.