Habari Mseto

Nilipata ufunuo 2006 ningeongoza Kenya, asema Rais Ruto

February 26th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

RAIS William Ruto, Jumapili, Februari 26, 2024 alisema kuwa alipata ufunuo mwaka wa 2006 kwamba angeiongoza Kenya kwa wakati mmoja.

Akihutubu kwenye mkutano wa maombi ulioongozwa na mwinjilisti Benny Hinn kutoka Amerika katika Uwanja wa Michezo wa Nyayo, jijini Nairobi, Rais Ruto alisema alipata ufunuo huo katika Mkutano wa Injili wa Asuza 100 nchini Amerika.

“Nitasema leo katika Uwanja wa Nyayo. Mara ya kwanza nilipopata ufunuo kwamba ningekuwa Rais wa Kenya ilikuwa 2006, wakati wa Tamasha la Asuza 100 nchini Amerika. Nilikuwa kwenye mkutano huo na mke wangu pamoja na watu wengine wengi,” akasema.

“Sikuamini kwamba mtoto kutoka Sugoi siku moja angekuwa rais wa Kenya.”

Rais alisema kuwa ana imani kuwa Mungu atatoa ufunuo mwingine mkubwa kwa Kenya, ili kuiwezesha kuwa taifa kubwa duniani.

“Tayari, ninaona Kenya litakuwa taifa kubwa duniani katika siku zijazo. Sababu kuu ni kuwa tunamwamini Mungu Aliye Hai,” akasema.

Wakati huo huo, alieleza alifanya mkutano na Balozi wa Amerika nchini, aliyemwambia Rais Joe Biden amemwalika kwa ziara rasmi ya kiserikali.

“Alikuja kuniambia; ‘unajua Rais wa Amerika amemwalika Rais wa Kenya kwa ziara ya kiserikali’. Ni ziara ya kipekee. Kwa muda wa miaka 20, hakuna kiongozi yeyote wa Afrika amefanya ziara ya kiserikali nchini Amerika,” akasema.

Viongozi wengine waliokuwepo kwenye mkutano huo wa maombi ni Naibu Rais Rigathi Gachagua, mkewe Rais Ruto-Bi Rachel Ruto na mkewe Bw Gachagua, Bi Dorcas Rigathi.