Uhasama Narok Kusini jamii mbili zikishambuliana
Na RICHARD MUNGUTI
UHASAMA mpya umeimbuka katika eneo linalokumbwa na ghasia za kikabila mara kwa mara Narok kusini baada ya wanaume watatu kufumwa mishale baada ya wizi wa mifugo.
Kulingana na Kamishna wa Kaunti ya Narok Bw George Natembeya jamii za Wakipsigis na Wamasai zilikabiliana Ijumaa usiku kufuatia wizi huo wa mfugo.
Bw Natembeya alisema jamii hizo zilishambuliana kufuatia wizi huo.
“Ghasia na makabiliano makali yalitokea baada ya wanaume watatu kuumizwa ghasia zilipozuka kufuatia wizi wa mifugo,” alisema Bw Natembeya
Kamshna huyo aliongeza , “Mtu mmoja alifumwa mishale Ijumaa usiku huku wengine wawili wakijeruhiwa katika kisa hicho.”
Afisa huyo wa utawala alisema ng’ombe mmoja aliibwa katika eneo la Ololoipang’i wakati wezi wa mifugo kutoka kabila moja walipovamia na kutoroka.
Kisa hiki kilizua mtafaruku katika vijiji vya Oloruasi na Nkoben vilivyojirani na Ololoipang’i.
“Vita vilianza mwendo wa saa nne usiku Ijumaa baada ya ng’ombe kuibwa. Wakazi walipiga kamsa na kuandama wezi hao ndipo makabiliano yakazuka na watu kujeruhiwa,” alisema kamishna huyo.
Waliohasiriwa walipelekwa hospitali ya kaunti ndogo ya Ololung’a na kufanyiwa upasuaji kutolewa mishale iliyokuwa imekwama kwenye miili.
Mnamo Septemba hali ilitokota kwa wizi moja huku makabiliano makali yakipelekea watu wanne kufa , mamia kuumizwa na nyumba zaidi ya 50 kuchomwa.
Tukio hilo la Ijumaa lilizuka siku moja tu baada ya Bw Natembeya kufutilia mbali kafiu (sheria ya kutotoka nje) ya miezi mitatu katika eneo la Olposimoru iliyoko Narok kaskazini.
Hata hivyo kamishna huyo wa kaunti alitoa wito kwa makabila mbali mbali yanayoishi humo waishi kwa amani na kujiepusha na uhasama.
Kamanda wa Polisi kaunti hiyo Thomas Ngeiywa alifichua kwamba polisi wameanzisha msako mkali kuwatia nguvuni waliopanga wizi huo uliosababisha mvurutano.
“Ng’ombe iliyoibwa ilipatikana na kurudishiwa mwenyewe. Hakuna haja ya kupigana tena bure kati ya jamii hizo mbili. Tumepokea taarifa zitakazotuwezesha kuwashika waliohusika,” alisema Bw Ngeiywa.
Wizi wa mifugo ndio umekuwa sababu kuu kwa jamii kukabiliana katika kaunti hiyo.
Mnamo Septemba makabiliano yalizuka katika eneo la Nkoben baada yam zee kuuawa na mbuzi wake 76 kuibwa. Wizi huo ulipelekea jamii ya Wamasai kuikabili jamii ya Wakipsigis.