Habari Mseto

Kesi ya kashfa ya transfoma feki yaanza

December 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

KUSIKIZWA kwa kesi ya ununuzi wa transfoma feki zilizopelekea kampuni ya Kenya Power (KP) kupoteza zaidi ya Sh408 milioni kulianza Jumatatu huku mahakama ikielezwa sheria za utoaji wa zabuni hazikufuatwa.

Bw Linus Ndege Mureithi (pichani juu) alimweleza hakimu mwandamizi Bw Felix Kombo kuwa uchunguzi aliofanya akishirikiana na Bw Jameson Namunyura uliumbua kasoro kadhaa.

Bw Mureithi alisema aliteuliwa na mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya ununuzi wa bidhaa za Serikali na mashirika yake Bw  Moris Juma.

“Tulikuwa tumeteuliwa tukiwa watatu lakini Bi Augusta Njue akajiondoa akidai mmoja wa wafanyakazi wakuu wa KP Bw Benson Muriithi waliyekuwa wakimchunguza ni mtu wa familia yao,” alisema Bw Mureithi.

Alisema uchunguzi ulichukua muda wa miezi miwili kisha akaandaa ripoti iliyopelekewa mkurugenzi wa uchunguzi wa jina (DCI).

Hakimu mwandamizi Felix Kombo. Picha/ Richard Munguti

“Je mlipata makosa yoyote mlipochunguza utoaji wa zabuni kwa kampuni ya Muwa,” akauliza kiongozi wa mashtaka Bw Alexander Muteti.

“Ndio, afisa ajulikanaye Imelda Bore aliteuliwa kushiriki katika kamati ya ufunguzi lakini hakushiriki. Afisa mwingine Joseph Atwoli alishiriki na hakuwa ameteuliwa na afisa mkuu wa KP Dkt Ben Chumo,” alijibu Bw Mureithi.

Bw Mureithi alisema kuwa utoaji wa zabuni hiyo ya ununuzi wa transfoma feki ulifanywa kiholela

Alisema kuwa alianza utenda kazi wake kwa kuchunguza Fomu zinazoalika makampuni yatakayoshiriki

Shahidi huyo wa kwanza kutoka kwa mamlaka ya ununuzi wa bidhaa za serikali (PRA) alisema zabuni iliyopewa kampuni ya Muwa Trading Company Limited haikufanywa kwa mujibu wa sheria.

Kiongozi wa Mashtaka Alexander Muteti. Picha/ Richard Munguti

Kabla ya shahidi huyo kuanza kutoa ushahidi mawakili walipinga naibu wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma (ADPP) Bw Alexander Muteti akitoa taarifa ya utangulizi.

Wakiongozwa na Bw Assa Nyakundi, Migos Ogamba, Harrison Kinyanjui , Andrew Makundi na Hiram Kago walisema “taarifa hiyo ya utangulizi itahujumu kesi dhidi ya washtakiwa hao 15.”

Lakini akitoa uamuzi hakimu mwandamizi Bw Felix Kombo alisema kuwa shera inaruhusu taarifa ya utangulizi kutolewa.

“Taarifa ya utangulizi sio ushahidi mbali in mukhtasari wa ushahidi utakaotolewa,” alisema Bw Kombo.

Hakimu alisema kuwa hakuna njia taarifa hiyo itashawishi mawazo ya mahakama mbali itaangazia tu ushahidi utakaowasilishwa.

Aliyekuwa mkurugenzi mkuu Kenya Power Dkt Ben Chumo (kulia) akiwa kizimbani na washukiwa wengine. Picha/ Richard Munguti

Akitoa taarifa hiyo Bw Muteti alisema kuwa ushahidi utawasilisha kudhihirisha jinsi wafanyakazi hao wakuu wa KP walikaidi sheria katika utoaji wa zabuni kwa kampuni ya Muwa iliyonunua transfoma feki na kupelekea zaidi ya Sh408 milioni kutoweka.

Bw Muteti alimweleza hakimu kuwa ushahidi upo jinsi Muwa iliishtaki KP katika mahakama kuu na ikalipwa zaidi ya Sh207 milioni.

Ushahidi huo , Bw Muteti alisema utachangia kuthibitisha makosa waliyofanya washtakiwa.

“Nitaomba hii mahakama ipitishe kifungo kikali dhidi ya Dkt Chumo , Beatrice Meso na wengine walioshtakiwa kwa kutumia mamlaka ya afisi zao vibaya na kulipa pesa za  umma kwa huduma zisizofaa,” alisema Bw Muteti.

Kesi inaendelea Jumanne.