Kimataifa

Rais wa zamani Tanzania Hassan Mwinyi kuzikwa Jumamosi

March 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MASHIRIKA

DAR-ES-SALAAM, TANZANIA

RAIS wa zamani wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, aliyeaga dunia Alhamisi jioni, atazikwa Jumamosi katika kijiji cha Mangapwani, Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mapema Ijumaa, marehemu atapelekwa katika Msikiti Mkuu wa Kinondoni Dar es Salaam, kabla ya kupelekwa nyumbani.

Mufti Abubakar Zubeir bin Ally anatarajiwa kuongoza sala hiyo, inayojulikana kama “Salat al-Janazah”, kama sehemu ya msingi ya ibada ya mazishi ya Kiislamu.

Baada ya maombi hayo mwili wake utapelekwa katika uwanja wa Uhuru ili kuwapa viongozi, wanadiplomasia na wananchi nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho kwa rais huyo mstaafu.

Waziri Mkuu alieleza zaidi kuwa jioni, mwili wa marehemu utasafirishwa kwenda Zanzibar kwa mazishi ya kitaifa yatakayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Rais huyo wa zamani alifariki akiwa katika hospitali ya Mzena Dar es Salaam baada ya kuugua saratani ya mapafu kwa muda.

Mnamo Alhamisi, Rais Suluhu aliagiza bendera ya Tanzania ipeperushwe nusu mlingoti kama njia ya kumpa Mwinyi heshima za mwisho.

“Ndugu wananchi, ni kwa masikitiko makubwa nakitangaza kifo cha rais mstaafu, aliyefariki saa kumi na moja na nusu jioni,” alisema Samia.

Novemba mwaka jana, rais huyo wa zamani alilazwa katika hospitali moja jijini London ila akarudi mjini Dar es Salaam kuendelea na matibabu.

Anakumbukwa kwa kuanzisha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi katika taifa hilo la Afrika Mashariki.