Walio ‘sober’ wakatazwa kupigania rasilimali chache za kuwafaa waraibu
NA KALUME KAZUNGU
UMARIDADI wa kituo cha kuwatibu waraibu wa dawa za kulevya, walevi wa pombe na uraibu mwingine katika Kaunti ya Lamu, umewasukuma hata wale ambao hawajaathiriwa na mihadarati kutaka angalau siku moja waishi kwenye taasisi hiyo.
Kituo hicho cha rihabu kilichoko eneo la Hindi na kilijengwa kwa kima cha Sh98 milioni, chini ya ufadhili wa Shirika la Msalaba Mwekundu.
Majengo yaliyoko kwenye kituo hicho yana mvuto na urembo wa aina yake, hali inayofanya wengi wanaopita karibu na kituo hicho kuvunjika shingo zao wakipinda kutazama mandhari ya mvuto wa aina yake ya rihabu hiyo.
Baadhi ya watu, hasa wageni, wamekuwa wakiulizauliza endapo majengo hayo ya rihabu ni nyumba za kukodisha, ikulu au makazi ya kifalme, hivyo kurai sana wasimamizi wa kituo hicho iwapo kuna nafasi ya kuishi pale wapewe angalau waonje utamu wa mandhari hayo.
Kituo hicho kilifunguliwa rasmi Aprili, 2019, dhamira kuu ikiwa ni kusaidia kukabiliana na janga lililokithiri la dawa za kulevya, hasa miongoni mwa vijana wa Lamu.
Rihabu hiyo ina uwezo wa kukimu mahitaji ya wanaotaka kubadilishwa tabia karibu 100 kwa wakati mmoja.
Taasisi hiyo huwabadilisha waraibu tabia kupitia kuwapa dawa mbadala au za kuwafanya watulie au za kutuliza neva zao, kuwashauri, kuwaelekeza, pamoja na kuwaandaa upya wakiwa wamefungiwa au kudhibitiwa kwenye mazingira hayo maalumu kabla ya kuachiliwa baada ya kipindi cha takriban miezi mitatu hivi ili kurudi kwa jamii yao wakiwa wametibika.
Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwa katika harakati za wasiokuwa waraibu wa dawa za kulevya kutaka kunufaika na huduma za taasisi hiyo, wengi wamekuwa wakimiminika kila kuchao kwenye rihabu ya Hindi kwa kigezo kwamba wapate angalau tiba kwenye hospitali iliyoko ndani ya kituo hicho.
Simon Mwangi, mkazi wa Hindi, anasema kila mara anapopatwa na maradhi amekuwa akivutiwa kuzuru hospitali ya rihabu ya Hindi, ambapo amekuwa akifaidi huduma za pale.
“Rihabu ya Hindi imejipanga vilivyo. Mbali na vitengo vya kawaida vya kuwarekebisha waraibu tabia, pia kuna hospitali pale. Mimi si mraibu lakini kikweli nimevutiwa sana na majengo ya rihabu ya Hindi. Nimekuwa nikitamani sana kuonja utamu wa majengo hayo na ndiyo sababu mimi kila wakati ninapougua hukimbilia pale kupata tiba kwenye hospitali yao. Mazingira na miundomsingi ya pale ni ya kuridhisha nafsi,” akasema Bw Mwangi.
Bi Anne Kyalo, mkazi wa kijiji cha Ndeu, tarafa ya Hindi, anasihi wasimamizi wa rihabu ya Hindi kuzingatia sana jamii inayowazingira, hasa zile familia zisizojiweza na kuzisaidia kupitia huduma zitolewazo pale, hasa zile za hospitali na ushauri nasaha.
Bi Kyalo alisisitiza kuwa badala ya kuangazia tu waraibu wa dawa za kulevya, wakati umewadia kwa rihabu ya Hindi kuruhusu kila mtu mwenye uhitaji wa ushauri nasaha kuingia pale ili kuhudumiwa.
“Kituo cha kuwarekebisha tabia waraibu na walevi cha Hindi kinapendeza. Najua mahali pale hawakosi kitengo cha ushauri nasaha. Wengi katika jamii wanapitia changamoto za kidunia zinazowafanya kuugua msongo ya mawazo, kiwewe, wasiwasi na mengineyo ya maisha ambayo ni hatari kwa afya zao. Turuhusiwe kuingia kituoni kupokea tiba ya ushauri nasaha,” akasema Bi Kyalo.
Hata hivyo baadhi ya wakazi, ikiwemo maafisa wa utawala waliozungumza na Taifa Leo waliwashauri wale wasiotumia dawa za kulevya kwamba haina haja wao kupigania rasilimali chache za kuwafaa waraibu kituoni.
Bw Abdalla Mohamed aliwasuta wanaotamani kuishi kwenye rihabu ya Hindi, akidai kuwa huko ni sawa na kujitakia mashaka.
“Wewe shukuru ulivyo sasa na mahali unapoishi. Usijisahau na kujipigia dua chafu. Unatamani au kuvutiwa na urembo wa majengo ya rihabu kiasi kwamba eti wataka siku moja na wewe uishi pale. Tambua kwamba hata wale walioko pale si kupenda kwao. Ni kutokana na mashaka na utumwa wa uraibu wa mihadarati wanaotaka kuuvua kupitia usaidizi wa rihabu,” akasema Bw Mohamed.
Ali Omar alishukuru Shirika la Msalaba Mwekundu kwa kuanzisha taasisi hiyo ya kubadilisha waraibu na walevi tabia, akisema ni yenye natija tele kwa jamii.
“Kama ni hospitali na zahanati nzuri nzuri na zenye mvuto, pia serikali yetu tukufu imejitahidi kuzijenga. Ya nini wewe usiyeathirika na dawa za kulevya kung;ang;ania hiyorasilimali kidogo ya rihabu ipasayo kuwafaa tu waathiriwa wa dawa za kulevya? Watu waache tamaa,” akasema Bw Omar.
Kwa upande wake aidha, Afisa Mshirikishi wa Msalaba Mwekundu, tawi la Lamu, ambaye pia ndiye msimamizi wa Rihabu ya Hindi, Bw Abdulhakim Abdul, alisema tangu kituo hicho kufunguliwa karibu miaka sita iliyopita hatua kubwa zimepigwa kufikia sasa.
Bw Abdul anasema waathiriwa wengi wa mihadarati waliopokea huduma kwenye taaisisi hiyo wameweza kubadilika na kwa sasa wanaishi vyema miongoni mwa jamii na familia zao.
Soma Pia: Sonko ashauri vijana Pwani wakae mbali na mihadarati
Anasema kati ya 2019 na 2023, jumla ya waraibu 161, wakiwemo wanaume 157 na wanawake wanne (4) wamepona uraibu baada ya kupitia huduma za rihabu hiyo ya Hindi.
“Kwa sasa tuko na wateja wapatao 14 wanaoendelea kupokea huduma zetu ili wanusurike kutoka kwa dawa za kulevya. Tumesaidia hata polisi na wanajeshi waliokuwa watumwa wa pombe, miraa na muguka kuacha uraibu huo na kwa sasa wanaishi vyema,” akasema Bw Abdul.
Lamu ni miongoni mwa kaunti za humu nchini ambazo idadi kubwa ya watu, hasa vijana wameathiriwa pakubwa na dawa za kulevya, hasa bangi, kokeni na heroni.
Baadhi ya miji inayotambuliwa kwa kuwa na idadi kubwa ya watumiaji wa dawa za kulevya ni kisiswa cha Lamu, Mbwajumwali, Siyu, Faza, Myabogi, Tchundwa, Kizingitini na viunga vyake.