• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 9:59 AM
Sonko ashauri vijana Pwani wakae mbali na mihadarati

Sonko ashauri vijana Pwani wakae mbali na mihadarati

NA ALEX KALAMA 

ALIYEKUWA Gavana wa Kaunti ya Nairobi Mike Mbuvi Sonko amewarai vijana eneo la Pwani kujitenga na utumizi wa dawa za kulevya.

Sonko amekiri kwamba uraibu huo umewaathiri pakubwa vijana wa eneo la Pwani na Kenya kwa ujumla na hivyo kuna haja ya mikakati zaidi kuidhinishwa katika jamii ili kudhibiti utumizi wa dawa hizo.

Akizungumza huko Miritini eneobunge la Jomvu, Kaunti ya Mombasa wakati wa pambano la kupimana nguvu kati ya bondia wa zamani wa Kenya Conjestina Achieng na Fatuma Zarika, Bw Sonko alisema yuko tayari kuwasaidia waraibu wanaotafuta nafuu ili kujiondoa katika janga hilo.

“Na mimi nasema vijana mambo ya mihadarati muachane nayo. Mnaona Conjestina sasa amepona amekuwa sawa… hata nyinyi tunaweza kuwafanyia hivyo. Hii safari si ya Conjestina peke yake… hii safari ni ya kuonyesha mfano kuwa kama tunaweza kusaidia Conjestina basi tunaweza kufanyia hivyo Mkenya yeyote yule,” alisema Bw Sonko.

Aidha gavana huyo wa zamani wa kaunti ya Nairobi alitaja kupona kwa Conjestina kutokana na utumizi wa dawa za kulevya na maradhi ya afya ya akili kuwa afueni kwa bondia huyo wa zamani wa taifa hili.

“Leo ndio siku yake ya kwanza anarudi tena ulingoni lakini tumekubaliana tukasema safari hii hatutamuachilia arudi tena kule Siaya. Tunamuandalia mazingira awe mkufunzi wa bondia,” alisema Bw Sonko.

Kauli ya kiongozi huyo iliungwa mkono na mkurugenzi mkuu wa kituo cha kuwahudumia wagonjwa wa afya ya akili na waraibu wa dawa za kulevya Amina Abdalla aliwasisitiza vijana kujiepusha na utumizi wa dawa za kulevya na ulevi kupindukia.

“Conjestina amekuwa hapa kwa mwaka mmoja na kwa sasa yuko sawa yuko tayari Conjestina kuonyesha talenta yake na kukuza talanta yake, kama vijana ombi langu ni kuwaambia vijana wetu tuache mambo ya mihadarati na tuweze kukuza talanta zetu,” alisema Bi Abdalla.

Ikumbukwe ya kwamba Conjestina amekuwa katika kituo hicho kwa kipindi cha mwaka mmoja akipokea matibabu baada ya kukumbwa na maradhi ya afya ya akili akiwa nyumbani kwao katika Kaunti ya Siaya.

  • Tags

You can share this post!

Tanzia: Mbunge Mary wa Maua apoteza meneja wake kupitia...

Gachagua ahofia maisha yake akidai makateli wa kahawa si...

T L