Hatutaki minofu, tunataka pombe, wazee wafoka
Na DENNIS SINYO
Mayanja, Bungoma
WAZEE watatu waliokuwa wakihudhuria sherehe ya kuwatoa wavulana jandoni, waliondoka kwa hasira walipoambiwa hakukuwa na pombe.
Inasemekana wazee hao walikuwa wamealikwa kuhudhuria hafla hiyo ili kuwashauri wavulana wakitoka jandoni baada ya kupashwa tohara.
Kulingana na mdokezi, mwenyeji wao alikuwa amemwagiza mkewe kuwaandalia pombe spesheli lakini agizo lake lilipuuzwa.
Wazee walipofika na kusubiri pombe. walimkabili mwenyeji wao wakidai alikuwa amewadharau.
“Tunataka pombe. Kama hakuna pombe hatuoni haja ya kukaa hapa’’alisema mzee mmoja.
Mama wa boma alidai kwamba alikuwa ameacha mambo ya pombe na kuwa kiongozi wa kanisa. “Nasikitika kwamba hakuna pombe ya wazee hapa. Mimi niliacha kutengeneza pombe baada ya kuwa kiongozi wa kanisa’’alisema mama wa boma.
Alidai alikuwa ameachana na maisha ya dunia kama kuandaa pombe baada ya kumjua Mungu.
“Kwa mwaka mmoja sasa, mimi ni kiumbe kipya. Mambo ya pombe niliachana nayo na kama mtaka kulewa, mjaribu kwingine,’’alisema mama huyo. Wazee hao waliombwa waingie kwenye chumba kimoja wafurahie minofu lakini walikataa.
Walidai haja yao kufika hapo ilikuwa ni pombe na haikuwa minofu. Wageni wengine walipokuwa wakimezea mate nyama ya kuku, ngombe, pilau na mapochopocho mengine, wazee hao walikuwa wamesimama chini ya mti wakitaka mvinyo.
“Baadhi yao walikuwa wametekwa na uraibu wa chang’aa huku wengine wakiwa wamebeba mirija ya kutumia kunywa busaa,” alisema mdokezi.
Inasemekana wazee hao waliondoka kwa fujo wakilaumu mama huyo kwa kuwaonyesha madharau.Walilalama walikuwa wametumia muda wao kwenye boma hilo na kama wangejua mapema, hawangefika hapo.
“Mimi mzee mzima naitwa hapa kushauri vijana ilhali hakuna pombe yangu?” aliteta mzee mmoja.