Makala

Mjue mbunge wa Maragua Mary wa Maua anayepigiwa upatu kuwania ugavana Murang’a

March 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 4

NA MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Maragua Mary wa Maua ameonekana akicheza siasa zinazojenga taswira ya mwanasiasa anayepanga mikakati na matayarisho ya kuingia mawindoni kusaka mnofu mkubwa.

Sasa kwa sauti za kichinichini, baadhi ya wakazi wanahisi Bi wa Maua analenga kuwania ugavana.

Amegeuka kuwa mfuasi sugu wa serikali ya Kenya Kwanza Alliance, ambapo hachelei kusisitiza kwamba imani yake iko thabiti nyuma ya Rais William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Katika harakati hizo, Bi wa Maua amekuwa akitoa kauli za kuonyesha wazi kwamba jicho lake kisiasa ni la anayelenga kupaa kutoka wadhifa wa ubunge ambao anahudumia kwa awamu ya pili sasa.

Alitishia kuwa angeongoza maandamano hadi ikulu ya Nairobi kumtaka Rais Ruto awape wenyeji wa Murang’a, na hasa eneobunge la Maragua, maji.

Soma Pia: Mbunge wa Maragua kuendea maji ya wakazi Ikulu

Huku siasa hizo zikichacha, alisema “ikiwa kwa uhakika gavana tuliyemchagua si muoga, tunataka kumuona akitatua suala hili la maji”.

“Tunataka kumuona akisimama ngangari na hata akijaribu kushinikizwa asikilize mitandao ya utapeli, akatae,” akawaka Bi Wa Maua.

Licha ya kauli hiyo, Gavana wa Kaunti ya Murang’a Irungu Kang’ata hakumjibu.

Wengi walidadisi kwamba mbunge huyo alikuwa amemwekea gavana Kang’ata mtego wa kumtaka azindue misururu ya majibizano ya kupimana nguvu.

Mbunge wa Maragua Bi Mary Wamaua akiwa katika kikao na waandishi wa habari katika Mkahawa wa Golden Palm mjini Kenol alipotishia kuongoza maandamano ya wakazi hadi Ikulu ya Nairobi kudai maji ya kunywa na ya unyunyiziaji kutoka kwa Rais William Ruto. PICHA | MWANGI MUIRURI

Naye Rais Ruto alipotua katika kaunti hiyo kwa ziara maalum mnamo Februari 15, 2024, aliamrisha Waziri wa Maji Zachariah Njeru ahakikishe kwamba matakwa ya mbunge huyo yameshughulikiwa mara moja.

Soma Pia: Rais atumia ‘mkato’ kuwapa wakazi wa Maragua maji

Mbunge huyo ndiye pekee katika Kaunti ya Murang’a ambaye amekumbatia vita dhidi ya pombe ya mauti na mihadarati kwa niaba ya Bw Gachagua ambaye kavitangaza wazi.

“Mimi ninaunga mkono juhudi zote za kupambana na ulevi pamoja na utundu wa baadhi ya polisi ambao ni washirika wa biashara za mauti. Kuna polisi ambao ni lazima waandamwe kwa kuwa wanauza bangi na hata kupokea hongo,” akasema.

Bi wa Maua aliambia Taifa Leo kwamba “kwa sasa ninawasaidia wakubwa wangu wa kisiasa ambao ni Rais Ruto na Bw Gachagua”.

“Hamu yangu ni kuona kwa pamoja na wakubwa wangu, tunatekeleza ahadi zetu za kabla ya uchaguzi ndipo ifikapo mwaka 2027, tujipate na wakati rahisi kuomba kura katika nyadhifa tutakazolenga,” akasema mbunge huyo.

Kuhusu mlipuko wa siasa za ubabe unaoendelea katika Kaunti ya Murang’a na Mlima Kenya kwa ujumla, Bi Wa Maua anasema kwamba ni muhimu kwa kila mtu kutekeleza majukumu yanayoambatana na wadhifa aliopewa.

“Wakati muafaka wa kuwindana na makubwa hayo ukifika, tutajitokeza tukawarai wapigakura watupandisha vyeo,” akaeleza.

Bi wa Maua pia ameonekana akilenga kuunganisha maeneo ya Kaskazini na Kusini mwa Murang’a ambayo humenyana kisiasa kwa uhasama mkuu.

Eneo la Kaskazini huwa na maeneobunge ya Kiharu, Kangema, na Mathioya huku Kusini kukiwa na maeneobunge ya Maragua, Kigumo, Kandara, na Gatanga.

Uhasama wa maeneo hayo ni kwamba, tangu ugatuzi uanze kufanya kazi mwaka 2013, eneo la Kaskazini ndilo limekuwa likitoa Gavana wa Kaunti.

Gavana mstaafu Mwangi wa Iria na Bw Kang’ata ni wa eneobunge la Kiharu.

Isitoshe, katika chaguzi za 2013 na 2017, eneo la Kaskazini ndilo lilitoa Gavana, Seneta na Mbunge Mwakilishi wa Kike huku eneo la Kusini likiachiwa ukoko wa Naibu Gavana.

Kwa sasa, Bi wa Maua anaonekana kuunganisha maeneo hayo mawili akitumia huduma za maji na kilimo cha unyunyiziaji ambapo amefanikiwa kumshawishi Rais Ruto kutoa amri kampuni ya maji ya Murang’a Kaskazini ihudumu hata ndani ya Kusini na hivyo basi kubomoa mpaka wa uhasama ambao hujidhihirisha kupitia Mto wa Maragua ambao hutenganisha maeneo hayo mawili.

Bi wa Maua aidha amekuwa akionekana akicheza siasa katika mipaka ya Kaskazini ambapo akiungana na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Murang’a Betty Maina, mbunge maalum Veronica Maina na diwani wa Kanyenyaini Bi Grace Nduta, wamezua sokomoko wakidai kwamba Bunge la Kaunti ya Murang’a liko na baadhi ya maafisa wa ‘team mafisi’.

“Kuna baadhi ya viongozi wa kiume wanawarushia mistari wenzao wa kike walio katika bunge hilo kwa mabavu na wakikataliwa, wanazindua njama za kuwahujumu waathiriwa,” akasema.

Wakati akitoa kauli hiyo, Bi Nduta alikuwa ametimuliwa kutoka bunge hilo la kaunti kwa msingi wa kuwazomea madiwani wenzake katika mitandao ya kijamii kuhusu “hali duni za huduma za afya katika hospitali za Kaunti ya Murang’a”.

Bi wa Maua alionekana kuchukua hatamu za kushirikisha kampeni hizo hadi akamwalika Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki katika hafla ya Kanisa eneobunge la Maragua alikomfahamisha kuhusu dhuluma dhidi ya viongozi wa kike.

Prof Kindiki aliamrisha Bi Nduta arejeshwe katika bunge hilo la Kaunti mara moja, akionya kwamba hakuna yeyote ambaye atakubaliwa kuhujumu utawala wa wanawake nchini.

Bi wa Maua anashikilia kwamba “hayo yote ni matukio ya kawaida kwa mwanasiasa wa haiba yangu na wakati muafaka ukiwadia, tutaweka wazi nia zetu kamili, kwa sasa ni kazi tu”.

Katika eneobunge lake, Bi wa Maua hufahamika vyema kwa kuwa mtumishi mashinani ambapo hutangamana na wenyeji na mara kwa mara akiwasaidia kutimua maafisa wa kiserikali hasa polisi ambao wanadhaniwa kuwa mafisadi.

Kituo cha polisi cha Sabasaba ambacho Kiko mita chache kutoka jengo lake la kibiashara na pia kilomita moja tu kutoka kwake nyumbani, ndicho ambacho maafisa wake hukipata kutoka kwa wa Maua.

Mara kwa mara huonekana akiwa katika kituo hicho akitoa malalamishi kuhusu uzembe, ufisadi na udhalimu.

Aidha, amekuwa katika mstari wa mbele kusifu maafisa ambao wamejitolea kuhudumia wenyeji kwa uadilifu.

Mwalimu wa shule ya msingi kitaaluma, Bi wa Maua alijiunga na siasa mwaka wa 2013 alipowania kiti cha Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a lakini akashindwa na Bi Sabina Chege.

Aliteuliwa kama diwani maalum ambapo mwaka wa 2015 aliandaa hoja ya kumtimua Gavana wa Iria na Bunge la Kaunti likaidhinisha kwa kura 34 dhidi ya 15 lakini ikakosa kupitishwa na Bunge la Seneti.

Mama wa watoto watatu, Bi wa Maua anarejelewa na Seneta wa Murang’a Joe Nyutu kama kiongozi imara ambaye hata akilenga kuwania ugavana, anaweza akafanikiwa.

“Mimi sio yule kiongozi wa kuzima ndoto za wengine. Bi wa Maua ndiye mbunge wangu kule nilikozaliwa na kwa uhakika, hatuwezi tukamkataa akituomba kura za ugavana. Hatuwezi tukazima dada yetu akilenga kuendelea kung’aa,” akasema Bw Nyutu.

Alisema kwamba kwa sasa wadhifa huo uko mikononi mwa Bw Kang’ata “ambaye pia ni mzalendo na shujaa wa Murang’a lakini tunajua watu wa Murang’a watarejea kwa debe 2027 kufanya uchaguzi mwingine”.

Bw Nyutu alisema kwamba kwa sasa Bi wa Maua amepata tajriba tosha ya kuhudumu kama Gavana baada ya kuwa mwalimu, diwani, na sasa mbunge.

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi anasema kwamba “aseme tu anataka huo ugavana na tutampa kwa kuwa sisi ni Kaunti ambayo inaamini uongozi wa kina mama sio kwa msingi wa kuwahurumia bali ni kwa kuwa wana uwezo kamili”.

Alisema kwamba Kaunti ya Murang’a imekuwa ikiafikia usawa wa kijinsia katika kuwachagua viongozi wa jinsia zote mbili pasipo hata kusukumwa na sheria.

[email protected]