Chiloba ateuliwa mkuu wa ubalozi mdogo wa Kenya jijini Los Angeles
NA WANDERI KAMAU
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (CA), Bw Ezra Chiloba, ameteuliwa na Rais William Ruto kuwa Mkuu wa Ubalozi Mdogo wa Kenya jijini Los Angeles katika jimbo la California nchini Amerika.
Kwenye taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Ikulu Hussein Mohammed mnamo Ijumaa, Bw Chiloba aliteuliwa kuwa mkuu wa ubalozi mdogo huo.
“Mheshimiwa Rais amewasilisha majina ya watu ambao wameteuliwa kama Mabalozi na Wawakilishi wa Kudumu kwa Bunge la Kitaifa ili kuzingatiwa na kuidhinishwa,” ikasema taarifa hiyo.
Kwenye orodha hiyo, Rais Ruto pia aliwateua washirika wake wa karibu wa kisiasa kama vile aliyekuwa Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi, aliyekuwa Seneta wa Kisumu Fred Outa, mbunge wa zamani wa Mugirango Magharibi Vincent Kemosi kati ya wengine.
Bw Maangi aliteuliwa kuwa balozi wa Kenya nchini Uganda, Bw Outa kama balozi nchini Misri, Bw Kemosi kama balozi nchini Ghana kati ya teuzi nyingine.
Uteuzi wa Bw Chiloba unajiri miezi michache baada ya kujiuzulu kutoka nafasi aliyokuwa akiishikilia katika CA, Oktoba 2023.
Tangazo hilo lilitolewa Oktoba 18, 2023, na mwenyekiti wa bodi ya CA Mary Mungai.
“Kwa niaba ya Mamlaka hii, namtakia kila la heri Mkurugenzi Mkuu anayeondoka. Tunamshukuru sana kwa mchango aliyotoa katika kuiboresha sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT),” akasema Bi Mungai.
Aliyekuwa msemaji wa Rais Ruto na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Afisi ya Rais, Bw David Mugonyi, aliteuliwa kujaza nafasi ya Bw Chiloba kama Mkurugenzi Mkuu wa CA.
Kabla ya uteuzi wake katika CA mnamo 2021, Bw Chiloba alikuwa amehudumu kama Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).