ODM itasalia imara hata bila Raila – Oparanya
NA SHABAN MAKOKHA
VIONGOZI wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) wamesema chama hicho bado kitabaki imara hata kama kinara wao Raila Odinga atachaguliwa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika.
Naibu kiongozi wa chama hicho, Wycliffe Oparanya na Katibu Mkuu Edwin Sifuna walitupilia mbali kasumba kuwa upande wa upinzani utasambaratika endapo Bw Odinga atachaguliwa mwenyekiti wa AU.Bw Sifuna alisema upinzani hautakimya Wakenya wakiumia.
“Ukisikia adui anakuombee mema unapoondoka kwa safari nzito uwe mwangalifu. Wengine wanadhani Raila akichaguliwa katika wadhifa huo basi upinzani utakuwa umekufa lakini wamekosea,” alisema Bw Sifuna.
Alieleza kuwa Bw Odinga alisema upinzani hautasambaratika kwani watu kama Bw Oparanya watachukua mamlaka. Bw Oparanya alifafanua kuwa uwepo wa upinzani haumhusu Bw Odinga bali unakubalika kikatiba.
“Yeyote asidhani endapo Bw Odinga ataondoka, upinzani uvunjike. Kwa kweli, Addis Ababa iko karibu. Bw Odinga anaweza kuja Nairobi wakati wowote na kurejea kazini,” akasema Bw Oparanya akiahidi kupeperusha bendera ya upinzani.
“Nitakuwepo kwenye kinyang’anyiro cha urais 2027,” akaongeza Bw Oparanya.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala aliwataka viongozi wa Azimio kuwa waangalifu na siasa na maneno yao dhidi ya chama cha Rais Ruto ambacho kinaunga mkono azma ya Bw Odinga ya kuwania uenyekiti wa AU.
Akizungumza wakati wa mazishi ya Timothy Khamala, babake Mbunge wa Lurambi Titus Khamala, Bw Malala alisema kwamba viongozi wachache wa Azimio walikuwa wakirusha cheche za maneno ilhali Bw Odinga anasaidiwa na UDA.
“Tunajua nyinyi ni upinzani lakini saa kama hii mnafaa kutulia kwani muungano wetu umeamua kuushikilia muungano wenyu. Hivyo ni vyema tuweke tofauti zetu kisiasa kwa manufaa ya Bw Odinga,” alisema.