Maswali mkulima wa kahawa akipata mamilioni, maelfu wakikosa tabasamu
NA MWANGI MUIRURI
NI hali ambayo inaweza tu kutafsiriwa kama muujiza shambani kwa mkulima wa kahawa kutoka Kaunti ya Busia ambaye amejipa pato la Sh2 milioni kutoka kwa hazina ya ustawishaji kahawa (CCARF).
Na sio yeye tu, kuna wengine wanne kutoka Kaunti ya West Pokot ambao wamepata Sh750, 000, kila mmoja akijipa Sh187, 500, ikiwa ilinuiwa wagawane kwa usawa.
Isitoshe, mwingine mmoja kutoka Homa Bay amejipa Sh100, 000 huku wa Nakuru akijipa Sh56, 000.
Muujiza ni kwamba, hazina hiyo ya CCARF iliyozinduliwa 2019 kwa makusudi ya kuinua wakulima wa kahawa kuafikia malengo ya uzalishaji kupitia vyama vyao vya ushirika.
Hakuna chama cha ushirika cha kahawa nchini ambacho kimeundwa na mkulima mmoja hivyo basi kuzua hali ya muujiza kuhusu jinsi wakulima hao walijipa hela hizo katika mpangilio ulioko.
Hazina hiyo hudhibitiwa na Ushirika wa wakulima wa Kahawa wa New KPCU na Benki ya Cooperative.
Katika ripoti iliyotolewa Machi 8, 2024 na New KPCU, hazina hiyo kufikia Machi 4, 2024 ilikuwa imetoa Sh3.7 bilioni kwa wakulima 298, 000, hiki kikiwa ni sawa na kiwango cha Sh12, 416 kwa kila mmoja.
Ndiyo sababu inazua gumzo kupata mkulima mmoja ambaye alijipa Sh2 milioni akiwa peke yake kwa mujibu wa ripoti hiyo na pia ushirika wa mkulima mmoja.
Ripoti hiyo inaonyesha Kaunti ya Nyeri imevuna Sh607.24 milioni kwa wakulima wake 68, 000 nayo Kirinyaga ikifuata kwa kujipa Sh478.3 milioni kwa wakulima 55, 000.
Kaunti ya Kiambu ni ya tatu ikiwa na Sh408.4 milioni kwa wakulima 21, 000 nayo Kericho ikiwa na Sh401.2 milioni za kugawia wakulima 20,232.
Murang’a ni ya tano kwa kuwapa wakulima 15, 148 jumla ya Sh343 milioni, nayo Machakos ikiwa ya sita kwa kuwapa wakulima 23,000 jumla ya Sh259.4 milioni.
Kaunti ya Embu ni ya saba kwa Sh248 milioni zikiwaendea wakulima 49, 000 huku wakulima wa 18, 000 Bungoma wakijizolea Sh247 milioni.
Kaunti ya Nandi ni ya tisa kwa wakulima 8, 000 ambao walijipa Sh181.05 milioni nayo ile ya Meru ikifunga orodha ya 10 bora kwa kuzoa Sh179.12 milioni kwa wakulima 10, 000.
Kaunti zilizoorodheshwa katika malipo ya hazina hiyo ni 24.
Licha ya kwamba hazina hiyo ilikuwa ya kukopwa na wakulima pasipo riba, isipokuwa asilima tatu ya utekelezaji, serikali imeamua kuitumia kama ya kulipa wakulima baada ya soko kuharibika.
Kizungumkuti kilizuka wakati serikali iliondoa leseni za madalali na pia ya wakulima kuuza kahawa yao moja kwa moja kukazuka ukosefu mkuu wa soko ambao uliishia wakulima kukaa mwaka mzima bila malipo.
Kwa sasa, Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ametangaza kwamba serikali iliongeza Sh4 bilioni kwa hazina hiyo ambayo ilikuwa na Sh2.74 bilioni.
“Kutoka kwa hazina hiyo ambayo sasa imetinga Sh6.74 bilioni ndipo tutapata pesa za kulipa wakulima kahawa yao kwa kiwango cha Sh80 kwa kilo ili kahawa iliyokwama kwenye maghala ikiuzwa, iwe ni kwa bei ya juu tuwaongeze masalio na pia tuwalipe bonasi mwisho wa mwaka,” Gachagua akasema.