Habari Mseto

Mcheshi Kiengei atangaza kuunga mkono Gachagua kukabili pombe haramu Mlima Kenya

March 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

MCHESHI maarufu, Muthee Kiengei, mnamo Jumapili, Machi 10, 2024, alitangaza kuunga mkono Naibu Rais Rigathi Gachagua kwenye juhudi zake kukabiliana na pombe haramu katika ukanda wa Mlima Kenya.

Mcheshi huyo—ambaye pia huitwa Pasta Ben Gathungu- alisema kuwa ni muhimu viongozi wa kidini kujiunga na Bw Gachagua na mkewe, Bi Dorcas Gachagua, kukabiliana na pombe hizo “ili kuokoa vijana katika ukanda huo”.

Bw Gachagua amekuwa akiongoza juhudi za kukabiliana na uuzaji na matumizi ya pombe hizo, akisema kuwa zinatishia kumaliza vijana na wanaume katika eneo hilo.

Akiongoza ibada ya maombi katika kanisa lake la Jesus Christ Compassion Ministries (JCM), Kaunti ya Kiambu, Bw Kiengei alisema kwamba kuna haja kubwa kanisa lijiunge na serikali katika kukabili ueneaji wa pombe hizo, kwani washirika wake ni miongoni mwa watu wanaoathiriwa nazo.

“Kanisa haliwezi kufunga macho na kujifanya halijaathirika na maafa ambayo yamekuwa yakisababishwa na pombe haramu. Binafsi, nimewazika watu wengi waliofariki kutokana na athari za pombe haramu. Wakati umefika viongozi wa kidini waunge mkono juhudi zinazoongozwa na serikali, hasa Naibu Rais Rigathi Gachagua,” akasema Bw Kiengei.

Akaongeza: “Mnamo Ijumaa, Machi 8, 2024, nilizungumza na Bw Gachagua na kumuahidi kwamba kama kanisa, tutaungana naye kwenye vita hivyo. Sitajali ikiwa watu watasema uamuzi huo una misukumo ya kisiasa. Nitatoa magari ya kanisa hili kuzunguka katika sehemu tofauti eneo la Kati kusisitizia wenyeji kuhusu athari za matumizi ya pombe haramu.”

Kauli ya mcheshi huyo ilionekana kushangaza wengi, kwani amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Kenya Kwanza.

Hata hivyo, amejitetea dhidi ya madai hayo, akisema kuwa kama kiongozi wa kidini, jukumu lake ni kulainisha viongozi, hasa wanapokosea.

Tangazo lake linaonekana kuwa hatua kubwa kwa juhudi za Bw Gachagua, ikizingatiwa hakuna kiongozi mwingine wa kidini ambaye amejitokeza kutangaza kumuunga mkono.

Mwezi uliopita (Februari 2024), watu 17 walifariki katika Kaunti ya Kirinyaga baada ya kunywa pombe haramu.