Habari Mseto

Maafisa sasa wachunguza madai ya ugonjwa hatari wa zinaa

December 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na ELISHA OTIENO

WAHUDUMU wa matibabu katika Kaunti ya Migori wanajitahidi kuzima uvumi kuhusu ugonjwa mpya wa zinaa, ingawa wameshindwa kuthibitisha kuwepo kwake.

Ugonjwa huo uliobandikwa jina ‘jakadala’ umesemekana kuua waathiriwa wanaoambukizwa kwa wiki moja pekee.

Wakazi wanadai ni ugonjwa uliogunduliwa katika maeneo ya uchimbaji madini ya Nyatike, Rongo, Awendo na Suna.

“Hatujaona mwathiriwa yeyote wa Jakadala…maafisa wangu wako mashinani wakijaribu kuthibitisha ukweli kuhusu kuwepo kwa ugonjwa aina hiyo wa zinaa,” akasema Waziri wa Afya katika kaunti hiyo, Dkt Iscar Oluoch.

Aliongeza: “Kile ambacho tumeshuhudia ni kansa ya sehemu nyeti, na hiyo ni tofauti na Jakadala ambayo kila mtu anazungumzia. Tunaomba kama kuna mwathiriwa yeyote ajitokeze katika hospitali zetu ili akaguliwe na kutibiwa.” Sawa na kaunti nyingine za Homa Bay, Kisumu na Siaya, Kaunti ya Migori ina idadi kubwa ya watu walioathiriwa Ukimwi.