Bei ya matumbo yapanda ghafla
NA MWANGI MUIRURI
HUENDA mahasla mtaani sasa wawe wakionja nyama kwa wali wa bwerere wa Naibu Rais Rigathi Gachagua baada ya bei ya matumbo kupanda ghafla.
Katika eneo la Mlima Kenya, kilo moja ya matumbo ambayo hayajapikwa ni Sh300 hadi Sh500 kutoka kwa bei ya zamani ya kati ya Sh130 na Sh200.
Bei ya nyama ya mutura pia imepanda ambapo mutura wa Sh10 uliokuwa awali unashikika kwa sasa unapimwa saizi ya pete ya uchumba, lakini wauzaji wakisisitiza kwamba ule wa bei chini ni Sh20.
Hali hii sasa imesemwa kuchangia pakubwa upenyo wa nyama ya punda katika soko na ambapo wateja hawaonekani kujali kuiendea hata kwa misitu na kingo za mito.
Mwenyekiti wa muungano wa mabucha ukanda wa Mlima Kenya Bw David Mwangi aliambia Taifa Leo kwamba hali hiyo imetokana na wizi wa mifugo unaodidimiza idadi ya mifugo wa kuchinjwa, gharama za juu za uchukuzi na nyongeza tele za ushuru.
“Gharama za uzalishaji mifugo kwa wakulima zimekuwa zikipanda kwa kasi kupitia bei za juu za chakula cha mifugo, na ili kujikinga dhidi ya hasara, wakulima wanaongeza bei ya mifugo huku nasi tukisaka faida, inatubidi tuongeze bei kwa wateja wetu,” akasema Bw Mwangi.
Bei ya kilo moja ya nyama ya ng’ombe imepanda hadi Sh600 na Sh700 kutoka kwa Sh500 na Sh600 nayo bei ya kilo ya nyama ya mbuzi ikipanda kutoka kati ya Sh650 na Sh750 hadi kati ya Sh800 na Sh900.
Bei ya nyama ya kuku wanaokatakatwa vipandevipande mtaani imepanda kutoka kati ya Sh20 na Sh50 hadi kati ya Sh30 na Sh60 huku katika hoteli, bei ya kipande robo cha mnofu wa kuku ikipanda kwa kati ya asilimia 20 na 40. Katika hoteli za kiwango cha kadri nyama nzima ya kuku iliyopikwa vizuri ikaiva, bei mpya ni kati ya Sh1,400 na Sh1,600.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaungama kwamba hali hiyo ni miongoni mwa sababu nyingine nyingi ambazo zinafanya walio katika pato la chini kuzidisha kilio kwamba utawala wa Rais William Ruto hauwajali.
“Ukitaka nchi ikukaidi, wazimie raia chakula, raha na ngono. Hapo sasa hutapata wa kukuimbia sifa,” akasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Prof Ngugi Njoroge.