• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
UTALII: Nani aliwaua ndovu 11 kwa sumu Maasai Mara?

UTALII: Nani aliwaua ndovu 11 kwa sumu Maasai Mara?

NA GEORGE SAYAGIE

HALI ya sintofahamu bado inaendelea kuzingira vifo vya ndovu 26 katika mbuga ya Maasai Mara inayosimamiwa na serikali ya kaunti ya Narok miezi mitatu iliyopita.

Ingawa chanzo cha vifo hivyo bado ni kitendawili, zaidi ya ndovu 11 kati ya idadi hiyo wanadaiwa walilishwa sumu.

Mwezi Novemba pekee, sababu ya vifo vya ndovu saba zilitajwa kama ‘zisizojulikana’ lakini kulikuwa na ushahidi kuashiria kwamba vifo vyao vilitokana na kula sumu kulingana na ripoti ya Mradi wa ndovu wa Mara(MEP) iliyochapishwa wiki jana.

Ripoti hiyo iliyochapishwa Disemba 14 kwenye mtandao MEP na mtandao wao wa Facebook inasema kwamba huenda ugomvi kati ya binadamu na wanyama ulichangia wanyama hao kupewa sumu.

Uchunguzi wa awali hata hivyo ulionyesha kwamba baadhi ya ndovu waliofariki waliwekewa sumu aina ya kemikali ya Cyanide. Hii ina maana kwamba walilengwa kwa kuvamia mashamba ya wakulima ama wawindaji haramu walilenga kutwaa pembe zao.

“Sasa kuna ushahidi uliopatikana kutokana na eneo la tukio na sababu za vifo hivi zilitokana na sumu baada ya kuvamia mashamba ya wakulima. Vile vile vifo vingine vilitokana na sumu ya kemikali ya kuwaua wadudu,” ikasema sehemu ya ripoti hiyo.

Watafiti wanashuku kwamba jamii za eneo hilo haswa wakulima wa mimea waliwapa sumu ndovu hao ambao walikuwa kero kubwa kwa kuyavamia mashamba yao.

“Tunatafuta ushahidi kwamba sumu ilitumika kuwaua wanyama hao. Mambo mengine tutayapata yanajumuisha iwapo dawa ya kuwaua wadudu iliptakana katika chembechembe za damu mwilini mwao na kuchangia vifo vyao,” ikaongeza ripoti hiyo.

Hata hivyo Afisa Mkuu Shirika la Huduma kwa Wanyamapori kaunti ya Narok Dickson Ritan alikataa kuzungumzia ripoti hiyo akisema wao hawakuhusika katika kutolewa kwake.

“Sisi si sehemu ya ripoti hiyo japo unaweza kuwapigia Msemaji wa KWS jijini Nairobi aliyejukumiwa kujibu maswala kama hayo,” Bw Ritan akasema kupitia mazungumzo ya simu. Hata hivyo juhudi za kufikia msemaji huo Paul Masela hazikufua dafu kwa kuwa hakupokea simu.

Hata hivyo serikali ya kaunti ya Narok ilikemea ripoti hiyo na kushangaa jinsi MEP ilivyoafikia idadi ya ndovu waliofariki na kuhoji iwapo ina jukumu lolote la kutekeleza kuhusu mbuga hiyo na mbona haikuwashirikisha katika utolewaji wake.

“Tuliwapigia simu Jumapili kuhusiana na ripoti yao na taarifa zaidi kuhusu hilo litatolewa baadaye,” akasema Afisa Mkuu Msimamizi wa mbuga ya mara Moses Kuyioni.

Ripoti hiyo ya kundi la kuwatunza ndovu inajiri wakati uhasama kati ya bindamu na wanyama unaendelea kutokota katika kaunti za Laikipia na Narok. Baadhi ya wakulima wanaoendeleza kilimo chao kando ya mto Enkare wamelazimika kuacha shughuli hiyo kutokana na vamia vamia za ndovu wanaoharibu mimea yao kila siku.

You can share this post!

Uasin Gishu kununulia wazee wa vijiji sare kwa Sh10 milioni

Kenya kunufaika na mradi wa kuweka intaneti vijijini

adminleo