Huenda wanasiasa walindwe na ‘askari rungu’ 2019
NA COLLINS OMULO
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Walinzi wa Kibinafsi Fazul Mohamed amefichua kwamba mpango wa kuwapa mafunzo walinzi hao ili waweze kumiliki bunduki na kuwasaidia polisi kutoa ulinzi kwa viongozi unaendelea
Bw Mohamed alifichua kwamba tayari mtaala ulioidhinishwa kimataifa umeundwa kuongoza mafunzo hayo yatakayozinduliwa mwaka ujao na mamlaka hiyo kwa ushirikiano na Taasisi ya mafunzo na elimu(TVET) na Mamlaka ya Kitaifa ya Mafunzo ya Kiviwanda(NITA).
“Tupo katika hatua za mwisho mwisho za mafunzo na TVET na NITA. Tumetuma maombi rasmi na kuwaleta wataalam wanaopitia mtaala huo. Kufikia mwisho wa mwaka, kila moja wenu atakuwa amepokea mafunzo hayo,” akasema Bw Mohamed wakati wa mkutano na walinzi wote wa kibinafsi jijini Nairobi.
Hatua hiyo inajiri baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i kuagiza mamlaka hiyo kuanzisha mafunzo hayo baada ya kutangaza kwamba walinzi wataruhusiwa kumiliki bunduki kama mojawapo za njia za kusaidia polisi kupigana na uhalifu.
Bw Matiang’i wakati huo alidai kwamba mpango huo ungeanza kutekelezwa mara tu baada ya kuundwa kwa mtaala na kanuni za kuuongoza.
Kulingana na Bw Mohamed, walinzi hao watapata mafunzo, kisha wapitie ukaguzi mkali na kukabidhiwa majukumu mazito ya kiusalama ndipo wapate cheti na leseni zinazotambuliwa kimataifa kutoa huduma za usalama zitakazowaruhusu kumiliki bunduki.
Baadhi ya majulumu hayo yatakuwa ni kutoa ulinzi kwa watu mashuhuri na kulinda fedha zinazosafirishwa benkini na bidhaa nyingine muhimu zinazowavutia wahalifu.
Hata hivyo walinzi hao hawataruhusiwa kuenda na bunduki hizo nyumbani ila wataziacha kwa kampuni wanazofanyia kazi ambazo pia lazima ziwe na hifadhi bora kwa silaha hizo.