• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Aliyekuwa mlinzi wa Mutula Kilonzo Jr apatikana na hatia

Aliyekuwa mlinzi wa Mutula Kilonzo Jr apatikana na hatia

Na PIUS MAUNDU

MAHAKAMA moja ya Makueni Jumatano ilimpata mlinzi wa zamani wa Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior na hatia, kwenye kisa cha ufyatulianaji risasi mnamo 2014 ambapo watu kadhaa walijeruhiwa.

Tukio hilo lilifanyika katika majengo ya Bunge la Kaunti ya Makueni.

Bw Shadrack Kioko Malekya, ambaye ni afisa wa polisi wa utawala alikuwa ameshtakiwa pamoja na polisi wengine watatu ambao walikuwa walinzi wa wanasiasa kadhaa katika kaunti hiyo.

Hata hivyo, mahakama iliwaondolea makosa Ndunda Muthoka, Mackline Francis na Nicholas Musyoka. Polisi hao walihudumu kama walinzi wa Spika wa zamani Stephen Ngelu, aliyekuwa Kiongozi wa Wengi Francis Mutuku na aliyekuwa mbunge wa Kaiti, Richard Makenga.

Kupitia Hakimu Mkuu Mkazi James Mwaniki, mahakama iliagiza kwamba walinzi hao wote waliufyatulia risasi umati wa watu ambao ulikuwa umekusanyika katika majengo ya bunge hilo. Hata hivyo, alisema kuwa Bw Kioko alimjeruhi Bw Brian Mutua bila kukusudia.

“Shadrack Kioko amepatikana na hatia ya makosa sita kwamba mnamo Septemba 23, 2014 katika majengo ya Bunge la Kaunti la Makueni akiwa na wengine walimjerihi Brian Mutua,” akasema hakimu.

Licha ya hayo, mahakama ilieleza kuwa walinzi hao walikuwa na haki ya kufyatua risasi, kwani umati ulioandamana na Gavana Kivutha Kibwana ulihatarisha usalama wa wanasiasa hao.

Hakimu pia hakubainisha aliyewajeruhi waathiriwa wengine, miongoni mwao Douglas Mbilu, anayahudumu kama Spika.

Watu wengine waliopata majeraha ya risasi ni Yakob Abdirazak, Francis Mutisya, Festus Nyamai na William Kinoti, aliye mlinzi wa Prof Kibwana.

Walinzi hao walifyatua risasi kumzuia Prof Kibwana na ujumbe wake kuingia bungeni, kwenye mkutano ulioandaliwa na wanasiasa wa eneo hilo.

Wanasiasa hao hawakumtaka Prof Kibwana kuhudhuria.

You can share this post!

KANU yamtaka Ruto kuomba Moi radhi

2007/8: Wengi waliolipwa fidia baada ya machafuko walikuwa...

adminleo