Habari Mseto

Tana River katika njia panda ikikosa wafanyakazi walioelimika

December 20th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na STEVE ODUOR

USIMAMIZI wa Kaunti ya Tana-River una wingi wa hofu kutokana na uhaba wa wafanyikazi waliohitimu.

Serikali hiyo imelazimika sasa kutafuta watu kutoka nje ya kaunti ili kushikilia nafasi mbalimbali za ajira.

Gavana Dhadho Godhana alisema serikali yake imejikakamua kuajiri watu wengi kutoka katika kaunti hiyo, lakini wengi wa waliotuma maombi hawajahitimu kimasomo.

Bw Godhana alisema kaunti hiyo haina watu wengi wa kuajiriwa katika nyadhifa tofauti za haiba. Alisema hayo wakati wa ibada katika Kanisa la Kenya Methodist, Hola, Jumanne.

Alikiri kuwa katika nyadhifa zilizotangazwa hivi majuzi, imekuwa vigumu sana kuzijaza na watu kutoka kaunti hiyo.

“Tumejaribu kujaza nafasi kadhaa kwa kuwaajiri watu wa eneo hili lakini cha kushangaza ni kuwa watu wetu hawajahitimu kimasomo,” alisema.

Alisisitiza kuwa maombi mengi yaliyotumwa hayakufikia mahitaji yote ili kutekeleza baadhi ya majukumu, hivyo usimamizi wake utatafuta waajiriwa wa kutoka nje kwa lengo la kutimiza malengo yake ya utenda-kazi.

Alisema vijana wengi katika kaunti hiyo wanatafuta kazi ya kuwa askari wa kaunti kwa kukosa masomo ya juu. “Lazima tukuze kesho ya kaunti hii kwa kuajiri watu wanaoelewa uzito wa majukumu watakayotekeleza,” akaongeza.

Lakini tumechanganyikiwa kwa sababu hawamo, huenda tukatafuta watu kutoka nje,” alisema.

Alisema kuwa usimamizi uliomtangulia pia ulikabiliwa na changamoto kama hiyo na kuulazimisha kuajiri watu wasio na viwango vya elimu vilivyohitajika.

Kutokana na hilo, kulikuwa na makosa mengi na uharibifu wa pesa za umma.

“Ni tatizo kama hili lililopelekea serikali iliyotangulia kuajiri watu wasio na ujuzi, hivyo, kukosa kuendelea. Hatuwezi kuenda njia hiyo na kutarajia kufanya vyema,” alisema.

Aliwaomba wakazi wa eneo hilo kwenda shuleni ili kuwa na uwezo wa kupata nafasi kubwa kubwa siku zijazo.

Asilimia 56 ya wakazi wa eneo hilo hawana elimu rasmi, hivyo Kaunti ya Tana River haiwezi kulinganishwa na kaunti zingine jirani.

Watalaam wakongwe wamepanga mkutano kujadili jinsi ya kubadilisha hali kwa lengo la kuiwezesha kaunti hiyo kuendelea.