Habari Mseto

Kinaya Babu Owino akitishia kupeleka maandamano Nyeri  

March 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

MNAMO Alhamisi, mbunge Babu Owino (Embakasi Mashariki) alitishia kupeleka maandamano katika Kaunti ya Nyeri, ikiwa serikali ya Kenya Kwanza haitapunguza gharama ya maisha kwa Wakenya.

Akihutubu kwenye mazishi ya babake mbunge Benjamin Gathiru (Embakasi ya Kati) katika eneo la Mukurwe-ini, Nyeri, Bw Owino alisema kwamba ataelekeza maandamano katika eneo hilo, kwani wakulima ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakilalamikia kudorora kwa bei za mazao yao.

Alisema kuwa ni kinaya kwa wakulima kulalamika, ilhali watu wengi katika eneo hilo waliipigia kura serikali ya Kenya Kwanza, chini ya uongozi wa Rais William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Hata hivyo, Bw Gachagua alimkosoa vikali Bw Owino, akisema hawezi kufaulu kuongoza maandamano katika eneo hilo, kwani “kushiriki maandamano si njia ya wakazi wa eneo hilo kutatua matatizo yao”.

Kauli ya Babu Owino

“Ikiwa serikali ya Kenya Kwanza itashindwa kutatua suala la gharama ya maisha, basi nitatoa maandamano Nairobi na kuyaleta hapa Nyeri, ili kuishinikiza serikali kupunguza gharama ya maisha. Inasikitisha kuwa wakulima ni miongoni mwa Wakenya ambao wamejitokeza kulalamikia kudorora kwa bei za mazao yao.”

Naibu Rais Rigathi Gachagua naye alimjibu akimwambia, “Maandamano si mtindo wa watu wa eneo hili kuelezea malalamishi yao. Panapozuka jambo lolote, huwa wanaketi chini na kujadili kuhusu njia za utatuzi. Kwa hivyo, hatutakuruhusu ulete maandamano hayo kwa watu wetu.”