Habari Mseto

Nogesha ngoma chumbani, mchepuko si suluhu

March 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANDISHI WETU

BAADHI ya watu wanalia kwamba ndoa zao zimekosa raha kwa kuwa wake au waume wao wamezembea chumbani.

Wanalalamika kuwa wachumba wao hawawakolezi raha ya tendo la ndoa walivyotarajia kabla ya ndoa.

Kinachofanya mtu afurahie sana mapenzi kwenye ndoa ni uzito wa hisia, urafiki wa dhati na uwazi kati ya wanandoa.

Sifa hizi zikikosa, hautafurahia mapenzi na tendo la ndoa.

Nasisitiza kuwa kinachokufanya ufurahie tendo la ndoa ni uhusiano mzito wa kihisia, jinsi kila mmoja anavyomjali mwenzake, heshima mliyonayo kwa kila mmoja, utu wema, upole, uvumilivu na unavyomfikiria mtu wako.

Masuala mengine yanayosaidia ni kuwa huru na karibu na kila mmoja, kutokuwa na siri baina yenu.

Vilevile, kuwa na uwezo wa kujiachilia kabisa na kuzingatia uhalisia wako bila kuona aibu mbele ya mwenzi wako ni mambo yanayoboresha uhusiano.

Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia kuwa wapenzi au wanandoa huhitaji kuwa na hakikisho la penzi- kujua kweli kuwa wanapendwa kwa wao kujitolea kikamilifu kwa penzi na uhusiano huo.

Wakati mwanamke anahisi kupendwa, kukubalika kabisa, kusikilizwa na kueleweka, yeye hujitolea kupenda na hufurahia kila sehemu ya mapenzi.

Mwanamume anapoheshimiwa sana, kupendwa, kueleweka na kutunzwa, huwa anachangamka na kutaka kufanya mapenzi na mkewe kila siku lakini wakati upendo wa kweli, ukaribu wa kina na uwazi unapokosa, nafasi yake huwa inachukuliwa na ubaridi, maumivu, kuchanganyikiwa ukosefu wa nguvu za kutekeleza tendo la ndoa na kila aina ya matatizo yanayoshuhudiwa katika ndoa.

Hali ikiwa hivi, wanandoa hubadilika kuwa chombo cha ngono tu cha kila mmoja wao.

Tendo linakosa maana yake. Linakosa kuwa burudani na kuwa mchezo wa kawaida tu mume akitaka kutimiza haja zake bila kujali hisia za mwenzake.

Mke anabadilisha mume kuwa chombo cha kumshughulikia bila kufurahia tendo.

Suluhu ya hali hii sio kutafuta burudani nje ya ndoa wanavyofanya baadhi ya watu huku wakijuta kuingia katika ndoa au kwa nini walichagua wake au waume wao.

Wengi wanapofikia hapo, hujipata wakianza michepuko, hali ambayo huishia kuwa ya kuwadhalilisha. Wengi hawafahamu kuwa hiyo si suluhu.

Wanachofaa kufanya ni kuangalia tatizo linalochangia mapungufu yao ni lipi na sio kuanza kudandia kila apitaye.