Askofu asihi Rais kuingilia kati kusuluhisha mgomo wa madaktari
NA BRIAN OCHARO
ASKOFU Mkuu wa Dayosisi ya Mombasa Kanisa la Katoliki Martin Kivuva ameitaka serikali kufanya mazungumzo na madaktari ili kupata suluhu na kusitisha mgomo unaoendelea.
Askofu Kivuva amesema muafaka unapaswa kupatikana ili kuokoa Wakenya wanaohangaika kupata matibabu.
wanaogoma ili kuokoa maisha ya Wakenya.
Akihutubia wanahabari katika Kituo cha Mitume huko Tudor, Askofu Kivuva alielezea wasiwasi wake kwamba misimamo mikali inayochukuliwa na serikali na muungano wa madaktari nchini (KMPDU) itazidisha mateso kwa wananchi wanaotegemea vituo vya afya vya umma.
“Hatuwezi kupata suluhu ikiwa pande zote mbili zitaendelea kushikilia msimamo mgumu. Tunatoa wito kwa pande zote mbili kulegeza kamba ili kuafikiana kuhusu suala hili la mgomo wa madkatari,” alisema Askofu huyo ambaye aliongoza waumini wa Kikatoliki katika kuadhimisha Jumapili ya Mitende, Machi 24, 2024.
Askofu aliongoza waumini wa Katoliki katika msafara kutoka eneo la Makupa kuelekea Kituo cha Mitume, Tudor.
Aidha, alikumbusha serikali kuhusu ahadi zake kuimarisha huduma za afya kwa Wakenya na kuweka kipaumbele maendeleo ya raia wanaochangia pakubwa ustawi wa taifa kupitia ushuru wanaotoa kwa utawala wa Kenya Kwanza.
Askofu Mkuu Kivuva alisisitiza kuwa ni kwa njia ya mazungumzo yenye maana pekee ndipo mvutano uliopo kati ya serikali na madaktari unaweza kutatuliwa.
“Mazungumzo ndio njia bora kila wakati. Naamini suluhisho linaweza kufikiwa. Tunaiomba serikali isijipige kifua,” alisema.
Viongozi wa kidini wana wasiwasi kuhusu mvutano kati ya serikali na madaktari, wakisema unaweza kuathiri mamilioni ya watu wanaotegemea vituo vya afya vya umma kupata matibabu.
Askofu Kivuva anapendekeza serikali isiweke imani yake kwa viongozi wenye misimamo mikali kuangazia mgomo wa madaktari, na badala yake itumie wanaoelewa mahangaiko ya madaktari na Wakenya ili kupata suluhu.
“Kama kanisa, wasiwasi wetu ni sawa na wa wananchi wa kawaida – tunataka madaktari warudi kazini na kuwe na dawa za kutosha hospitalini. Ikiwa kuna mgomo katika hospitali za umma, ni raia wa kawaida wanaoumia. Wanategemea vituo vya afya vya umma kwa huduma za matibabu,” alielezea.
Isitoshe, anamtaka Rais William Ruto kusikiliza ombi la mamilioni ya Wakenya wanaomtegemea kufanya uamuzi wa busara kwa manufaa ya wananchi.
Mgomo wa madaktari nchini kote sasa umeingia siku ya 12 bila dalili zozote za pande zinazozozana kuafikia makubaliano.
Wiki iliyopita, Wizara ya Afya na KMPDU, walifanya kikao cha mazungumzo ambacho hakikuzaa matunda.