Urais Senegal: Faye amlemea mgombea wa ‘deep state’
DAKAR, SENEGAL
MGOMBEA urais wa upinzani nchini Senegal Bassirou Diomaye Faye, anatarajiwa kutawazwa rais mpya wa taifa hilo baada ya mwaniaji wa Muungano wa serikali Amadou Ba kukubali kushindwa.
Kulingana na matokeo yasiyo rasmi ya uchaguzi wa urais uliofanyika Jumapili Faye alikuwa anaongoza kwa asilimia 53.7 za kura huku Ba akiwa na asilimia 36.2.
Hii ni baada ya kura kutoka asilimia 90 za vituo vya kupigia kura kuhesabiwa baada ya awamu ya kwanza ya upigaji kura, tume ya uchaguzi ilisema Jumatatu.
Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa na Mahakama ya Rufaa Ijumaa wiki hii.
Awali siku hiyo, Jumatatu, Ba ambaye aliungwa mkono na Rais anayeondoka Macky Sall, alimpigia simu Faye na kumpa pongezi, msemaji mmoja wa serikali aliwaambia wanahabari.
“Kwa kuzingatia hesabu za matokeo ya uchaguzi wa urais kufikia sasa na tunaposubiri tangazo rasmi, nampongeza Faye kufuatia ushindi wake katika awamu ya kwanza ya uchaguzi,” Ba akasema.
Ba ni waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo.
Rais wa Senegal Macky Sall pia alimpongeza Faye, 44, akiutaja ushindi wake kama “ushindi wa demokrasia ya nchi ya Senegal.”
Sall, ambaye hakuwania baada ya kukamilisha mihula yake miwili inayoruhusiwa kikatiba, pia alielezea kufurahishwa na jinsi uchaguzi huo uliendeshwa kwa njia huru na haki.
Wagombeaji wengine pia walikubali ushindi wa Faye Jumatatu usiku akiwemo Anta Babacar Ngom, mgombeaji wa kipekee wa kike.
Faye alijitosa katika ulingo wa siasa za Senegal zaidi ya wiki iliyopita baada ya kuachiliwa huru kutoka gerezani pamoja na kiongozi wa upinzani na mlezi wake Ousmane Sonko.
Sonko alizuiwa kushiriki uchaguzi huo kama mgombea urais kwa kosa la kuwaharibia jina viongozi wakuu wa serikali ndiposa akampendekeza Faye awanie.
“Kumbuka kuwa siku 10 zilizopita Faye alikuwa gerezani. Alikaa huko kwa zaidi ya miezi 11 kwa kuweka ujumbe katika Facebook ambao serikali ilifasiri kuwa ulichochoa uhaini. Sasa amegeuka kutoka mfungwa wa kisiasa hadi kuwa rais mtarajiwa wa Senegal,” mwanahabari mmoja akasema.
Wapigakura
Mamilioni wa raia wa Senegal walishiriki katika uchaguzi huo wa Jumapili kumchagua rais wa tatu wa taifa hilo la Afrika Magharibi.
Shughuli hiyo ilitangulizwa na misukosuko ya kisiasa pamoja na maandamano ya kupinga serikali yaliyodumu kwa miaka mitatu.
Raia wengi walielezea kuchukizwa kwao na utawala wa Rais Sall kwa kushindwa kuwaondolea hali ngumu ya kiuchumi.
Japo Faye hajaongea hadharani tangu alipopiga kura yake Jumapili, wafuasi wake wanasema ushindi wake umetokana na uungwaji mkono kutoka kwa Sonko.
Faye na Sonko waliendesha kampeni pamoja chini ya kauli mbiu, “Diomaye mooy Sonko” (Diomaye ni Sonko), wakiahidi kupambana na ufisadi na kutoa kipaumbele kwa maslahi ya kiuchumi ya raia.
Kwa hivyo, wapiga kura walishawishika kuwa kumpigia kura Faye ilikuwa sawa na kumpigia kura Sonko aliyezuiwa kuwania urais.
Faye alipata umaarufu mkubwa miongoni mwa wapigakura wa umri mdogo nchini Senegal ambapo zaidi ya asilimia 60 ya watu wenye umri wa miaka 25 kwenda chini wanahangaika kwa kukosa ajira.