Wazee wataka matambiko kumtakasa Mzee Kibor
Na TITUS OMINDE
BARAZA la wazee kutoka jamii ya Wakalenjin linatafuta mbinu za kumtakasa na kumpatanisha mkulima na mwanasiasa mtatanishi katika kaunti ya Uasin Gishu, Bw Jackson Kibor na wake zake baada ya kuwataliki .
Wazee hao walizungumza na Taifa Leo baada ya mahakama ya Eldoret kumpa Kibor kibali cha kumtaliki mkewe wa tatu waliokaa pamoja kwa ndoa kwa miaka 43.
Talaka hiyo imetolewa miezi 15 baada ya kumtaliki mke wa pili mnamo Oktoba 6, 2017.
Kulingana na wazee hao, tabia ya Mzee Kibor ni mwiko kwa jamii ya Wakalenjinkufanya matambiko ya kutakasa jamii.
Mwenyekiti wa baraza la Myoot, Meja mstaafu, John Seii alisema tabia hiyo ni hatari kwa kizazi cha jamii hiyo.
Mzee Seii alimtaka Bw Kibor kunyenyekea na kusikiza ushauri wao ili kupata mwafaka na kuwa na heshima kama mzee.
“Kwetu kama jamii ni laana kutaliki mama wa umri wa miaka 70 baada ya kushirikiana naye kutafuta mali kama ilivyo kwa mzee Kibor,” alisema Meja Seii
Bw Seii alimtaka Mzee Kibor kufikiria upya kuhusu hatua yake huku akisema jamii haitamruhusu kutesa wake wa zaidi ya miaka 50.
Kwa mujibu wa wazee hao ni kwamba wanawake hao wana haki ya kumiliki mali husika na kuishi katika boma zao bila kusumbuliwa na mzee Kibor
“Unafukuza mama wa miaka 70 aende wapi hii ni laana nani ataoa yeye?Tunaona aibu kushauri watoto kwani wanatuuliza nini mbaya na mzee Kibor,” alisema Mzee Seii
Pia walikosoa mahakama kwa kutozingatia hali ya wakongwe hao.
Kwa mujibu wa mzee Philip Barno ni kwamba ingekuwa afueni iwapo mahakama ingeshauri Kibor kutengana kwa muda badala ya kuwapa talaka huku wakisema kuwa sheria inaruhusu korti kutoa ushauri kwa wananchi kutafuta suluhu mbadala ali maaruuf ADR.
“Mahakama ingeshauri Kibor kutumia mbinu mbadala kutafuta suluhu la utata wa ndoa yake,kutaliki wake wawili kwa muda wa miezi 15 ni aibu na fedheha kubwa kwa wazee,” alisema Mzee Philip Barno
Bi Naomi Jeptoo Kibor ambaye ni mke wa hivi punde kutalikiwa na Kibor alitilia mkazo kwamba hatakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama huku akitkaa wazee kushawishi Kibor kutomfurusha kutoka katika makazi yake eneo la Ziwa kaunti ndogo ya Soy.
“Sitakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama kile ambacho naomba wazee ni kushauri kibor asinifurushe kutoka katika makazi yangu bali aache niendele kuishi hapa nikingojea siku ya kufa kwangu kwnai mimi ni mzee sina mahali pakwenda,”alisema mama huyo alipotembelewa na Taifa Leo nyumbani kwake.