Habari Mseto

Nyakundi aamriwa kufuta picha za Steve Mbogo mitandaoni

December 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na  RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu imemwamuru mwanablogu Cyprian Nyakundi afute katika mitandao ya kijamii habari alizoandika kuwahusu mwanasiasa Steve Mbogo na mkewe.

Jaji Jacqueline Kamau aliamuru Bw Nyakundi afute habari alizosambaza katika mitandao ya Twitter , Facebook na mtandao wake kuwahusu wawili hao.

Jaji Kamau alitoa agizo hilo baada ya Bw Nyakundi kukosa kufika kortini kujitetea kwamba mnamo Oktoba alisambaza habari za kuwakejeli Bw Mbogo na mkewe .

Bw Mbogo aliyewania kiti cha Starehe wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 2017 alimshtaki Bw Nyakundi akisema “alichapisha habari za uwongo zilizolenga kumharibia familia yake.”

“Endapo mshtakiwa hatazuiliwa na hii mahakama ataendelea kusambaza habari hizi za uwongo zinazolenga kuniharibia sifa na jina langu kama mwanasiasa na pia mfanyabiashara mstahiki,” alisema Bw Mbogo.

Bw Mbogo aliyebwagwa katika uchaguzi wa mwaka uliopita na Njagua Kanyi alimshtaki Bw Nyakundi na kuomba mahakama iamuru amlipe fidia ya Sh20 milioni.

Akitoa uamuzi wake , Jaji Kamau alisema mshtakiwa alikosa kufika mahakamani licha ya kuamriwa awasilishe ushahidi kujitetea.

“Hii mahakama imezingatia malalamishi ya Bw Mbogo na mkewe. Ni kweli habari zilizochapishwa katika mitandao ya kijamii imewaharibia sifa,” alisema Jaji Kamau.

Aliendelea kusema, “Naamuru zifutwe kabisa”.

Jaji alisema kuwa mshtakiwa amewaharibia sifa Bw Mbogo na mkewe.

Mahakama iliamuru kesi hiyo itajwe tena Januari 24 ndipo walalamishi waeleze jinsi wameharibiwa majina yao.