TAHARIRI: Waliomaliza shule washikwe mikono
NA MHARIRI
HABARI kuwa watahiniwa zaidi ya 400,000 wa mtihani wa kitaifa wa kidado cha nne (KCSE) mwaka huu walipata alama ya ‘D+’ hadi ‘E’ inazua maswali tele kuhusu ubora wa elimu nchini.
Cha kuvunja moyo zaidi ni inakuwaje baada ya miaka 12 shuleni watahiniwa 30,000 wanapata alama ya ‘E’ kumaanisha hawakuelimika hata kidogo licha ya kuwa shuleni muda huo wote.
Takwimu hizi zinaonyesha kuwa viwango vya ubora wa elimu nchini ni vya kutiliwa shaka sana na inapasa wataalamu wa elimu, Serikali, wazazi na walimu kuanza kujiuliza maswali kuhusu hali hii.
Ingawa haimaanishi kuwa waliopata alama hizo za chini ni wajinga ama ni watu ambao wamefeli maishani, ukweli ni kuwa kuna tatizo linalohitaji utatuzi wa haraka.
Hii ni kwa sababu wengi wa watahiniwa hawa hawataweza kupata nafasi za kuendelea na masomo yao, bila kusahau kuwa hawakupata maarifa yoyote ya kujiendeleza kimaisha iwapo watakatiza masomo yao hapa.
Ingawa Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa wale watakosa nafasi katika vyuo vikuu wajiunge na vyuo vya kiufundi, ukweli ni kuwa vilivyomo haviwezi kutoshea vijana 400,000.
Matokeo yake ni kuwa mwaka ujao Kenya itakuwa na maelfu ya vijana ambao wameingia kwenye uchumi bila mbinu za kuchangia maendeleo, na hivyo itawabidi kutegemea familia zao kujikimu kimaisha.
Wengine walio na ujasiri wa kujisimamia kimaisha wataingia mijini kwa imani kuwa watapata ajira, lakini watapigwa na butwaa kupata hakuna kazi, hali ambayo huenda ikachochea wengi kuingilia uhalifu na mienendo inayokiuka maadili kama vile ukahaba, utapeli na kutumiwa kuuza mihadarati.
Hii ndiyo sababu Serikali inapasa kukubali ukweli huu na kutafuta sera na mbinu za kukabiliana na hali ya vijana wengi kumaliza shule kisha wanaachwa kutapatapa bila wa kuwapa mwongozo wa kujisimamia kimaisha.
Ingawa mtaala mpya unaanza kutekelezwa mwaka ujao, bado kuna idadi kubwa ya wanafunzi ambao wataendelea na huu wa sasa, kumaanisha kuwa maelfu zaidi watajipata katika hali ya kukumbana na ukweli wa kuwa katika taifa ambalo linawaacha waogelee bahari kuu kivyao licha yao kutojua kuogelea.