Mvulana aliyeugua ugonjwa wa kiajabu KCSE azoa alama ya B
Na CHARLES WASONGA
SHANGWE na vifijo vilitamalaki katika Shule ya Upili ya Kaewa iliyoko kaunti ndogo ya Kathiani, Kaunti ya Machakos baada ya mtahiniwa mmoja, aliyekumbwa na ugonjwa wa ajabu akiendelea kufanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE), kupata alama ya B.
Kulingana na mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bi Anne Njogu, mwanafunzi huyo kwa jina John Sila Mutunga alianza kufura mwili wake wote akiendelea kufanya mtihani na ikamlazimu amkimbize katika zahanati moja ya karibu kupokea matibabu.
Hata hivyo, wauguzi walishindwa kuutambua ugonjwa huo na kumshauri arejee shuleni.
“Mwanafunzi huyu alianza kufura mwili wake wote na ikanilazimu kuchukua hatua ya haraka. Nilimkimbiza hospitalini lakini ugonjwa uliokuwa umemwathiri haukubainika mara moja” asema mwalimu huyo.
Hali ilipozidi kuwa mbaya, mwalimu huyu asema kuwa alipigia simu wazazi wa Mutunga na wakafika shuleni haraka.
Hata hivyo, mama yake, Mueni Mutunga, alisema kuwa mtoto huyo alikuwa alianza kuugua mwaka uliopita, wakati wa likizo, ndipo akampeleka katika hospitali mbalimbali kupokea matibabu.
“Mtoto wangu alianza kukumbwa na ugonjwa huo wa ajabu mwaka jana na nikampeleka katika Hospitali ya Mbagathi na ile ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) kwa matibabu. Madaktari walisema alikuwa anaugua ugonjwa unaoitwa kwa kisayansi Renal Parenchymal.” asema mama huyu kwa majonzi.
Mama huyu alidokeza ya kwamba, licha ya kupewa dawa, mtoto wake alizidi kuathiriwa na ugonjwa huo, lakini ukapungua shule zilipofunguliwa.
Mutunga aliendelea na masomo yake kwa muda lakini baadaye mwili wake ulianza kuvimba tena alipokuwa akiendelea kufanya mtihani wa KCSE.
Mjomba wake, Kalama Muli aliambia Taifa Leo kuwa ugonjwa huo umewagharimu zaidi ya Sh100,000 wakimtafutia mtoto huyo matibabu lakini mpaka sasa hawajafanikiwa.
“Tumejaribu tuwezavyo kumtafutia mtoto huyu matibabu ya kuridhisha, lakini ugonjwa alionao umekosa utatuzi. Hata hivyo, tunamshukuru Mungu maana mvulana huyu amefana katika mtihani wa KCSE na kuwashtua wengi ” asema Kalama akiongea na waandishi hawa nje ya shule hiyo.
Kwa minajili hii, wazazi hawa wanaomba serikali, mashirika mbalimbali ama watu binafsi wajitokeze kuwafaa kwa hali na mali ili wamtafutie mvulana huyo matibabu ya hali ya juu kabla ya hali yake kudhoofika zaidi.
“Tumeuza sehemu ya mali ya familia ili tugharamie matibabu ya mtoto wetu, lakini hatujapata mafanikio yoyote. Twaomba wahisani wajitokeze kutufadhili ili tumtafutie mtoto huyu matibabu ya hali ya juu” akasema.