Mfanyakazi alivyombaka binti wa waziri hotelini
Na ERIC MATARA
MWANAMUME aliyedaiwa kumnajisi binti wa waziri mwenye umri wa chini ya miaka 18, Alhamisi alishtakiwa katika Mahakama ya Nakuru baada ya kukaa kizuizini kwa siku tatu.
Bw Reuben Kiborek alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Bi Yvonne Khatambi, ambapo alishtakiwa kwa kumdhulumu kimapenzi msichana huyo Desemba katika hoteli ya kifahari iliyo mjini Nakuru.
Kulingana na upande wa mashtaka, Bw Kiborek alimnajisi msichana huyo Desemba 23 hotelini kisha akatoroka kabla kupatikana na polisi baadaye.
Alikabiliwa na shtaka jingine tofauti la kumfanyia mtoto kitendo kichafu kinyume cha sheria katika siku hizo hizo hotelini humo.
Mshtakiwa huyo alikamatwa Jumatatu na kufungwa kwa siku tatu katika Kituo cha Polisi cha Bondeni kabla kufikishwa mahakamani jana.
Aliingizwa mahakamani kisiri kupitia mlango wa nyuma mwendo wa saa tano unusu asubuhi pengine kwa nia ya kuzuia wanahabari waliokuwa wamekita kambi nje ya korti wasimwone.
Punde alipofikishwa kizimbani, Bi Khatambi aliagiza “wanahabari wote na mtu yeyote ambaye si jamaa wa Bw Kiborek” waondoke mahakamani.
Wakati wote wa kikao kortini, aliziba uso wake kwa kutumia ukaya ili asipigwe picha.
Mshtakiwa aliyekuwa amesimama wima kizimbani alikanusha mashtaka na akaachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000 pesa taslimu na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.
Hakimu aliagiza kwamba kesi itajwe Januari 18, 2019 ili tarehe ya kusikilizwa kwake iamuliwe.
Baada ya kukanusha mashtaka, umati unaosemekana kuwa marafiki wake ulimzingira ili kuepusha wanahabari kumpiga picha kisha wakamwondoa mahakamani.
Bw Kiborek alikamatwa Jumatatu na maafisa wa kikosi cha Flying Squad ambao walimtafuta hadi Kaunti ya Baringo baada ya kisa cha unajisi kuripotiwa kwa polisi.
Alisafirishwa kwa gari hadi Nakuru ambapo alipelekwa katika kituo cha polisi cha Bondeni alikohojiwa na wapelelezi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai.
Mshukiwa huyo ambaye awali alitarajiwa kufikishwa katika mahakama ya hakimu Nakuru mnamo Jumatatu mchana, alihamishwa hadi katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Nakuru baada ya polisi kufahamishwa kwamba wanahabari walikuwa wanafuatilia kisa hicho.
Kufikia Jumatatu jioni, alikuwa hajashtakiwa na kuwepo kwake katika kituo cha Bondeni kuliwekwa siri hadi wakati aliposhtakiwa jana.
Ripoti za polisi zinaonyesha kuwa mshukiwa alimchukua msichana huyo kutoka nyumbani kwao Jumapili mchana.
Alimpeleka kwa gari hadi mjini Nakuru ambako ilisemekana waliingia katika hoteli ya kifahari inayotoza kati ya Sh14,000 na Sh50,000 kwa usiku mmoja, ambako inadaiwa alitenda uhalifu huo.