Habari Mseto

Wakenya walioazimia kufunga ndoa 2018 walinoa – Ripoti

December 28th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na VALENTINE OBARA

ZAIDI ya nusu ya Wakenya waliokuwa wamepanga kuoa au kuolewa mwaka huu waliambulia patupu huku ikiwa imesalia siku nne pekee kabla mwaka ukamilike, utafiti umeonyesha.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na shirika la Trends and Insights For Africa (TIFA), inaonyesha mwanzoni mwa mwaka huu, asilimia tisa ya Wakenya walikuwa na lengo la kufunga ndoa lakini kati yao, ni asilimia nne pekee waliofanikiwa.

Malengo mengine ambayo yalikuwa yametajwa na wananchi ni kuanzisha biashara ambapo asilimia 28 kati ya asilimia 52 waliokuwa na lengo hilo walifanikiwa, na kupata ajira mpya ambapo asilimia 11 kati ya 33 wenye lengo hilo walifua dafu.

Ripoti hiyo iliyotolewa jana, ilionyesha kuna asilimia 28 ya Wakenya ambao hawajaamua kuhusu malengo yao ya 2019, lakini wengi wanatazamia kuanzisha biashara, kupata ajira mpya, kuweka usawa kati ya kazi na maisha ya kijamii na kuendeleza elimu ya juu.

Kuna asilimia 10 ya wananchi wanaotaka kuoa au kuolewa mwaka huu.

Wakati huo huo, utafiti huo wa TIFA ulibainisha zaidi ya asilimia 90 ya Wakenya waliridhishwa, japo kwa viwango tofauti, na jinsi mitihani ya Kitaifa ya Shule za Msingi (KCPE) na ule wa upili (KCSE) ilivyosimamiwa mwaka huu.

Asilimia 36 walisema waliridhishwa huku asilimia 55 wakisema waliridhishwa sana. Kuna asilimia saba ambao hawakuridhishwa na asilimia mbili ambao hawakuridhishwa sana.

Masharti makali yalitumiwa kwenye usimamizi wa mitihani hiyo kutokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali hasa maafisa katika Wizara ya Elimu wakiongozwa na Waziri Amina Mohamed, na ile ya Usalama wa Ndani ikiongozwa na Dkt Fred Matiang’i.

Washukiwa kadhaa walikamatwa wakijaribu kushiriki kwenye wizi wa mitihani wakiwemo walimu, maafisa wa usalama na watahiniwa.

Idadi kubwa ya waliohojiwa walikuwa na umri wa kati ya miaka 25 na 34 (asilimia 29), wakifuatwa na miaka 18 hadi 24 (asilimia 28) na wenye zaidi ya miaka 45 (asilimia 25).