Habari Mseto

Bodi yafuta leseni ya daktari wa Cuba aliyekataa kazi Lodwar

December 28th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY LUTTA

BODI ya Wahudumu wa Matibabu na Madaktari wa Meno imefutilia mbali leseni ya daktari kutoka Cuba ambaye alikuwa amepelekwa kufanya kazi katika Hospitali ya Kaunti ya Rufaa ya Lodwar, Kaunti ya Turkana.

Bodi hiyo ilifutilia mbali leseni ya Dkt Ricardo Adolfo Sanchez Carrillo, ambaye alikuwa mpasuaji kwa kukosa kufika kazini alipohitajika hospitalini humo kisha baadaye akajiuzulu.

Hii ni licha ya mahitaji makubwa ya huduma za matibabu katika kaunti hiyo ambayo ilikuwa imetengwa kwa muda mrefu kabla ugatuzi kuanza kutekelezwa, ambapo wakazi walikuwa wakitegemea zaidi Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi iliyo Eldoret kwa matibabu maalumu.

Afisa Mkuu wa Afya na Usafi katika Kaunti ya Turkana, Bw Moses Natome, alithibitisha uamuzi huo.

“Alikuwa haji kazini kisha baadaye akaandika barua kibinafsi kwa bodi kwamba alijiuzulu na alitaka kuondoka nchini. Bodi ilifutilia mbali leseni yake ili asiweze kuhudumu kokote kwingine nchini,” akasema Bw Natome.

 

Dkt Ricardo alipelekwa katika hospitali hiyo Juni 30 pamoja na mwenzake, Dkt Rodgers Gonzalez, ambaye ni daktari wa kifamilia aliyesalia.