• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
2018: Muafaka wa Uhuru na Raila uliibua mtazamo mpya wa kisiasa bungeni

2018: Muafaka wa Uhuru na Raila uliibua mtazamo mpya wa kisiasa bungeni

Na CHARLES WASONGA

MBWEMBWE na mahanjam zilishamiri bungeni mnamo Machi mwaka huu Rais Uhuru Kenyatta alipowasilisha Hotuba yake kuhusu Hali ya Taifa.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa wabunge wa upinzani, haswa wale wa chama cha ODM, kumchangamkia Rais bungeni tangu alipoingia mamlakani kwa mara ya kwanza mnamo 2013.

Hali hii ilisababishwa na hatua ya Rais Kenyatta kusalimiana na Kinara wa Upinzani Raila Odinga mnamo Machi 9 na hivyo kumaliza uhasama wao wa kisiasa.

Katika hotuba iliyosheheni wito wa maridhiano, Rais Kenyatta aliwaomba Wakenya msamaha kwa maafa, ghasia na uharibifu wa mali ulioshuhudiwa kabla na baada ya chaguzi za Agosti 8 na Oktoba 26, 2017.

“Nawaomba nyie wabunge kusameheana kwanza kisha muwe mstari wa mbele kuwahimiza Wakenya wote waliotofautiana kutokana na siasa za mwaka jana wasameheane na kuishi kama ndugu na dada. Nawahimiza msalimiane na kupalilia amani na maridhiano jinsi mimi na ndugu yangu Raila tulifanya miezi mwili iliyopita,” akaeleza.

Rais Kenyatta alishangaa pale wabunge na maseneta waliohudhuria kikao hicho cha pamoja walipoanza kusalimiana na kukumbatiana kwa furaha pasina kujali miegemeo yao ya kisiasa.

Mbunge machachari Paul Ongili almaarufu Babu Owino, aliwashangaza wenzake aliponyanyuka kitini mwake na kumsalimia Rais Kenyatta kwa furaha.

Bw Owino, ambaye ni mbunge wa Embakasi Mashariki, aliwahi kutofautiana na Rais Kenyatta mara kadhaa kabla na baada ya chaguzi za mwaka jana ambapo mapema mwaka huu alikamatwa na kuzuiliwa korokoroni kwa siku tatu kabla ya kushtakiwa kwa kosa la kumtusi kiongozi wa taifa.

“”Kila mmoja wetu anapaswa kuomba msamaha kwa maneno makali na hasira za mwaka jana. Kutoka

Mandera hadi Maseno, kutoka Mbita hadi Mvita, kutoka Lodwar hadi Lunga Lunga, hebu tusalimiane na kukumbatiana na majirani zetu,” Rais alikariri katika hotuba yake, huku akishangiliwa na wabunge.

Alimsifu Bw Odinga kwa “kudhihirisha uzalendo” alipokubali kuweka kando tofauti za kisiasa kwa ajili ya kuunganisha taifa na kupalilia maridhiano miongoni mwa Wakenya.

Hotuba ya Rais Kenyatta pia iligusia hatua ambazo serikali yake imepiga katika mchakato wa kuendeleza maadili ya kitaifa, kutekeleza majukumu yake ya kimataifa na hali ya usalama nchini.

Kiongozi alielezea kujitolea kwa serikali yake kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni mwaka jana na hatua ambayo itachukua kuhakikisha kuwa Ajenda Nne Kuu za Maendeleo zimeafikiwa ndani ya kipindi cha miaka minne ijayo.

Ajenda hizo nne, ambazo zimeorodheshwa katika manifesto ya chama tawala cha Jubilee, ni Afya kwa Wote, uwepo wa chakula toshelezi, uimarishaji wa sekta ya utengenezaji bidhaa, na ujenzi wa nyumba 500,000 za gharama nafuu.

Tayari serikali imezindua mpango majaribio ya mpango wa afya kwa wote katika kaunti ya Kisumu. Pia utatekelezwa katika kaunti nyingine tatu.

 

You can share this post!

Bodi yafuta leseni ya daktari wa Cuba aliyekataa kazi Lodwar

2018: Uhamisho wa walimu ulizua utata baina ya KNUT na TSC

adminleo