Habari Mseto

Hofu washukiwa wa Shakahola wakianza tena mfungo gerezani

May 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA BRIAN OCHARO

WASHUKIWA watatu wa mauaji ya Shakahola, kwa mara nyingine tena wameanza mfungo hatari katika gereza la Shimo La Tewa ambapo wanazuiliwa.

Mahakama ya Shanzu iliarifiwa Jumanne kwamba washukiwa hao watatu, wote wakiwa ni wanawake, wameanza kufunga tena, na hivyo kuhatarisha uwepo wao katika siku za kusikizwa kwa kesi hiyo iwapo hawataamrishwa kula.

Kulingana na wakili wao, Bw Lawrence Obonyo, mmoja wa washukiwa hao yuko kwenye mfungo wa maombi huku wengine wawili wakilala njaa kulalamikia kudhulumiwa na wasimamizi wa gerezani hilo.

Hakimu Mwandamizi Leah Juma anayeshugulikia kesi hiyo ameiagiza usimamizi wa gereza la Shimo la Tewa kuwapeleka watu hao hospitalini kutibiwa na kuangaliwa afya yao.

Pia, Hakimu huyo aliamuru ripoti ya matibabu kuhusu hali yao ya afya iwasilishwe mahakamani hapo baadaye.

Hii si mara ya kwanza kwa washukiwa hao kuanza tena mfungo baada ya kuokolewa kutoka msitu wa Shakahola, ambapo mhubiri tata Paul Mackenzie na washirika wake wanadaiwa kusimamia mfungo uliosababisha vifo vya mamia ya wafuasi wa kanisa la Good News International.

Mwaka uliopita, kabla ya kufunguliwa mashtaka rasmi, washukiwa hao, akiwemo Mackenzie, walianza tena kufunga huku wakilalamikia kuwekwa kizuizini kwa muda mrefu bila kufunguliwa mashtaka, ukiukwaji wa haki zao na unyanyasaji magerezani.

Ilibidi upande wa mashtaka utafute amri ya mahakama kwa ajili ya kuwalazimisha washukiwa hao wale kilazima kuzuia hatari ya kufa kwa njaa gerezani.

Wakati huo huo, mahakama imepanga rasmi tarehe ya Mackenzie na washtakiwa wenzake 94 kukutana na mashahidi katika kesi hiyo ambapo wanakabiliwa na mashtaka 13 yanayohusiana na ugaidi.

Mashahidi katika kesi hii wataanza kuwasilisha ushahidi wao kuanzia Julai 8 hadi 11, na 22 hadi 25.

Hii inaashiria kuwa kesi hiyo itachukua muda wa siku nane mwezi Julai.

Hakimu Juma alisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati kwa washtakiwa wote, na kuwaagiza wahusika kuzingatia muda uliowekwa.

“Wahusika wote lazima wajitayarishe kuendelea; la sivyo, notisi itolewe kwa kila mtu mapema . Mhusika yeyote anayepanga kuwasilisha maombi lazima afanye hivyo mapema,”alisema Bi Juma.

Mackenzie, mkewe Rhoda Mumbua Maweu na wengine 93 wamekana makosa manne chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya 2012.

Mackenzie almaarufu kama Mtumishi, Nabii au Papaa, Bi Maweu, Smart Mwakalama na mkewe Mary Kadzo Kahindi na wengine 28 wameshtakiwa kwa madai ya kujihusisha na uhalifu wa kupangwa na hivyo kuhatarisha maisha na kusababisha vifo vya wafuasi 429 wa kanisa lao.

Mackenzie, Bi Maweu, Bw Kwakalama, mkewe na wenzake 28 pia wamefunguliwa mashtaka ya itikadi kali, ambapo serikali ilidai kuwa washukiwa hao waliendeleza mfumo wa imani uliokithiri kwa madhumuni ya kuwafanya wafuasi wao kufunga hadi kufa.

Zaidi ya hayo, Mackenzie na mkewe wameshtakiwa zaidi kwa kosa la kupatikana na vifaa vinavyohusiana na ugaidi, ambapo inadaiwa walipatikana na video , vitabu na vitu vengine vinavyotumika katika kuchochea vitendo vya kigaidi ambavyo ilihatarisha maisha ya waumini na wafuasi wa kanisa lake.

Serikali ilidai kuwa makosa hayo yalitokea katika eneo la Furunzi huko Malindi tarehe tofauti kati ya 2020 na 2023.

Kesi hiyo itatajwa tena Mei 29.