Mahakama yaachilia vijana wa TikTok walioigiza wizi mbele ya kituo cha polisi
NA MAUREEN ONGALA
WATENGENEZAJI maudhui wanne waliokamatwa Jumatano kwa kuigiza wizi nje ya kituo cha polisi wameshtakiwa kwa kuchapisha habari za uongo.
Washukiwa hao akiwemo kijana wa umri wa miaka 17, walikamatwa baada ya video hiyo kusambazwa pakubwa kwenye TikTok.
Mahakama imewapa wanne hao dhamana ya Sh200,000 na mdhamini wa kiasi sawa na hicho
Shabir Suleiman, Omar Juma, Caleb Kahindi na mvulana huyo mchanga ambaye hatuwezi kumtaja kwa sababu za kisheria, walikanusha mashtaka mbele ya Hakimu Mkuu wa Kilifi Ivy Wasike.
Kulingana na mashtaka, mnamo Mei 7, 2024, washukiwa hao pamoja na wengine ambao hawako kortini waliposti video kwenye TikTok akaunti @shabir-shirazy003 kwa jina “Wizi Nje ya Kituo cha Polisi Kilifi” ambayo walijua ni uongo.
Kesi hiyo itasikizwa Julai 30.
Kwenye video hiyo ya kuigiza, mwanamume ambaye anaonekana kuwa mlevi, anatoka kwenye mkahawa wa Kituo cha Polisi Kilifi na ‘akaibiwa’ mkoba wake na wanaume wawili waliokuwa kwenye bodaboda.
Kamanda wa polisi wa Kaunti ndogo ya Kilifi Kaskazini Kenneth Maina alisema kwenye mahojiano ya awali kwamba polisi walikamata washukiwa baada ya kuwatambua kupitia kwa kamera za mkahawa.
Video zaidi Taifa Leo iliyopata inaonyesha mmoja wa washukiwa akimfuata mhudumu wa usafi wa mkahawa huo ambaye baada ya kusemezana kwa muda mfupi alimpa ‘gota’.
Vijana hao walikamatwa wakiwa majumbani mwao Kilifi. Bw Maina anasema wangali wanasaka mshukiwa mwingine ambaye bado hajapatikana.