Habari Mseto

Mfanyabiashara ajipata pabaya kwa wizi wa Sh54.7m

May 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA alishtakiwa Jumatano kwa wizi wa zaidi ya Sh54.7 milioni kutoka benki moja jijini Nairobi.

Bw Daniel Mwangi Mucheru alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Ben Mark Ekhubi katika mahakama ya Milimani, Nairobi.

Bw Mucheru alikanusha kuiba pesa hizo kutoka Benki ya Guaranty miaka minne iliyopita.

Mfanyabiashara huyo aliyekamatwa kutoka eneo la Kasarani, Nairobi alidaiwa alitekeleza wizi huo kati ya Aprili 2 na Mei 29, 2020.

Pia alikabiliwa na shtaka la kula njama kuilaghai benki hiyo Sh54,700,000 akishirikiana na watu wengine ambao hawajafikishwa mahakamani kujibu kesi.

Kabla ya kusomewa mashtaka, wakili wa serikali Virginia Kariuki alimweleza hakimu kwamba kesi dhidi ya Bw Mucheru itaunganishwa na nyingine inayoendelea mbele ya hakimu mwingine.

“Bw Mucheru alikuwa anafikishwa kortini kusomewa mashtaka tu kisha apelekwe mbele ya hakimu aliyeorodheshwa kusikiliza kesi hii ndipo aombe dhamana,” Bi Kariuki alimweleza Bw Ekhubi.

Kiongozi huyo wa mashtaka aliomba kesi hiyo ipelekwe mbele ya hakimu anayesikiliza kesi dhidi ya washukiwa walioshtakiwa awali iunganishwe.

Bw Mucheru alikana aliiba pesa hizo kutoka tawi la Westlands la Benki ya Guaranty Trust Bank (Kenya) Limited iliyoko katika jengo la Skypark.

“Utaenda kuomba dhamana mbele ya hakimu anayesikiza kesi dhidi yako na washukiwa wengine,” Bw Ekhubi alimweleza mshtakiwa.

Polisi walimtia pingu Bw Mucheru na kumpeleka katika mahakama inayosikiliza kesi inayomkabili.