Habari Mseto

NYS hatarini kulipa deni la magodoro kwa lazima

May 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA JOSEPH OPENDA

SHIRIKA la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) huenda likalazimika kulipa madeni ya kampuni ya kutengeneza magodoro.

Hii ni baada ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Nakuru, Samuel Mohochi kutupilia mbali kesi inayohusu Sh68 milioni.

Kampuni ya Prime Mattresss Limited iliwasilisha kesi mahakamani dhidi ya NYS mnamo Machi 2018, ikidai shirika hilo limekataa kulipa deni la Sh68 milioni.

Kampuni hiyo ilipewa kandarasi na Wizara ya Utumishi wa Umma, Jinsia na Vijana mnamo Oktoba 15, 2013, kusambaza magodoro 10,000 kwa NYS kwa gharama ya Sh 3,250 kila moja.

Ingawa baadhi ya malipo yalifanywa na NYS kati ya 2015 na 2016, deni lililobaki halijalipwa tangu 2016, licha ya kampuni hiyo kulidai shirika hilo na hata kutoa notisi ya kulishtaki.

Kulingana na kampuni hiyo, hakuna pesa iliyopokelewa tangu 2016 kwani juhudi zote za kulisukuma shirika hilo kulipa deni hilo hazijafaulu.

“Licha ya notisi kutolewa, washtakiwa wamekataa kulipa deni lililotajwa,” ilisomeka sehemu ya ombi hilo.

Kampuni hiyo iliomba maagizo ya mahakama ya kuilazimisha serikali kulipa madeni hayo pamoja na riba iliyoongezwa.

Waliotajwa katika kesi hiyo ni NYS, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana, na Masuala ya Jinsia, na Mwanasheria Mkuu.

Wakati wa vikao vya awali, NYS ilikosa kufika kortini licha ya notisi nyingi kutolewa.

Bi Fronika Shirikah, wakili mkuu wa serikali, alijitetea akisema kuwa alikuwa likizoni wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo.

Kampuni ya Prime Mattresss Limited ilipinga ombi la NYS, ikidai kuwa shirika la NYS lilipoteza nafasi yake ya kushiriki katika kesi hiyo.