Habari Mseto

Raia wa Congo asukumwa gerezani kwa kashfa ya dhahabu ya Sh15m

May 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA imeagiza raia wa Congo anayeshtakiwa kwa kashfa ya dhahabu ya Sh15 milioni asalie gerezani hadi pale idara ya urekebishaji tabia itakapotoa ripoti kuhusu mienendo yake.

Hakimu mkazi katika mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi aliamuru Dally Poba Puati azuiliwe katika gereza la Industrial Area hadi Mei 16, 2024.

Bw Puati alishtakiwa Alhamisi kwa kumlaghai Bw Isa Mikail Muhammad takriban Dola 100,000 (Sh15 milioni) akidai alikuwa na uwezo wa kumuuzia kilo tano za dhahabu.

Shtaka lilisema kwamba Bw Puati akishirikiana na watu wengine, alikula njama za kumlaghai Bw Muhammad pesa kwa kisingizio angemuuzia dhahabu.

Hakimu alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka Virginia Kariuki kwamba Bw Puati alitekeleza uhalifu huo kati ya Agosti 1 na Septemba 1, 2023, katika mtaa wa Kileleshwa, Kaunti ya Nairobi.

“Umeshtakiwa kwamba ulimlaghai Bw Muhammad takriban Dola 100,000 sawa na Sh15,000,000 ukijifanya ungemuuzia kilo tano za dhahabu. Ni ukweli ama sio ukweli?” Bw Ekhubi alimwuliza mshtakiwa.

Akijibu Bw Puati alisema: “Mimi sijui chochote kuhusu dhahabu hiyo na mamilioni ya pesa. Sikuhusika kamwe. Naomba uniachilie kwa dhamana ndipo nikutane na wanaonishtaki siku ya kusikilizwa kwa kesi.”

Bw Puati aliomba aachiliwe kwa kiwango kisicho cha juu cha pesa akisema “mimi sina mapato”.

“Naomba hii mahakama iniachilie kwa dhamana,” akasema.

Mshtakiwa aliendelea kueleza mahakama kwamba atafika kortini wakati wa kusikilizwa kwa kesi inayomkabili.

Bi Kariuki hakupinga ombi la mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana ila aliomba cheti cha kusafiria cha Bw Puati kichunguzwe kwa vile majina hayafanani na pia hayalingani.

Hakimu aliamuru ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia iwasilishwe kabla ombi lake la kuachiliwa kwa dhamana kuamuliwa.

Mshtakiwa huyo aliomba apelekwe hospitalini akifichua sio buheri wa afya.