Habari Mseto

Vibiritingoma watano wanaodaiwa kuwaibia wanaume watimuliwa Makutano

May 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

VIBIRITINGOMA watano wanaodaiwa kuwaibia wateja wao, wametimuliwa kutoka mji wa Makutano ulioko Kaunti ya Embu.

Wanawake hao, kwa mujibu wa ripoti ya utekelezaji uamuzi huo, wanadaiwa kuwa wezi sugu.

Uamuzi wa busara wa kamati hiyo ni kwamba washukiwa hao walitambuliwa kila mmoja na nyumba yake, kisha wakatumiwa polisi na wanakamati wa Nyumba Kumi kuwafurusha kutoka ngome zao za kuwafurahisha wanaume wanaonunua mahaba.

“Wawili (ambao majina yao yametolewa) wana historia ya kuwa wezi katika miji ya Thika na Karatina huku mmoja akiwa aliachiliwa kutoka jela hivi majuzi,” ripoti hiyo yasema.

Mmoja naye inadaiwa kwamba alikuwa mwokovu na msanii wa nyimbo za Injili kabla ya kugeukia wizi na kujiuza kimwili.

Ripoti hiyo inaelezea kwamba watano hao walibainika baada ya kutajwa na mmoja wao ambaye hivi majuzi alikamatwa akiwa na simu ya wizi.

“Mshukiwa huyo alikamatwa katika chumba chake cha kupokea wateja wa mahaba na simu hiyo ikapatikana,” ripoti yaelezea.

Ripoti inaeleza zaidi kwamba kibiritingoma huyo naye alikuwa amepora simu hiyo kutoka kwa mshukiwa wa ujambazi ambaye alikuwa ameenda nayo Makutano kusaka mahaba baada ya kushambulia na kumjeruhi vibaya mmiliki wayo halali.

“Wachunguzi walimnasa mwanamume huyo na baada ya kumhoji alikopeleka simu, alidai kwamba iliporwa akiwa kwa kibiritingoma mmoja katika mji wa Makutano na ndipo baada ya kuvamia chumba cha kahaba huyo, tukapata simu hiyo,” polisi waelezea kwenye ripoti.

Ni katika kujaribu kusafisha nembo ya mji huo ulio katika mipaka ya kaunti za Kirinyaga, Murang’a na Machakos ambapo uamuzi uliafikiwa wa kuwatimua vibiritingoma ambao walitajwa kama wezi sugu.

Mji huo uko katika mzunguko wa barabara ya kuelekea Nyeri na Embu na jina lake maarufu ni Makutano ya kwenda mji wa Mwea ulioko katika Kaunti ya Kirinyaga ukielekea mjini Embu.

Ripoti hiyo inasema kwamba uchunguzi zaidi utaendelezwa wa kuwatimua washirika wote wa magenge katika mji huo.

“Mji huu ni ngome ya wezi wa kufyonza mafuta kutoka kwa magari ya uchukuzi na kisha kuyauza kimagendo, na walanguzi wa mihadarati. Pia umejaa waandalizi, wapakiaji na wasambazaji wa pombe haramu na pia majangili wa mtandao wa wizi wa mifugo,” ripoti hiyo yasema.