Habari Mseto

Mbunge awarai wanakandarasi kujenga madarasa, mabweni kwa ustadi

May 11th, 2024 1 min read

NA OSBORN MANYENGO

MBUNGE wa Kwanza, Ferdinand Wanyonyi, amewarai wanakandarasi wanaofanikisha ujenzi wa mabweni, madarasa na maabara katika taasisi za elimu kuafikia ubora uliowekwa na wataalamu wa ujenzi.

Eneobunge la Kwanza liko katika Kaunti ya Trans Nzoia.

Akihutubia wanahabari katika Shule ya Upili ya Wasichana ya St Francis Assiss Kolongolo baada ya kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa jumba la ghorofa kwa kima cha Sh21 milioni, Bw Wanyonyi alisema huwa ni jambo la kutamausha ikitokea jengo linaibua nyufa miezi michache baada ya kukamilika kujengwa kwa fedha za umma.

Mradi wa ujenzi katika Shule ya Upili ya Wasichana ya St Francis Assiss Kolongolo. PICHA | OSBORN MANYENGO

Jumba hilo litakuwa na vyumba vinane vya wanafunzi kusomea.

Bw Wanyonyi alisema pesa za umma zinafaa kulindwa na kutumika jinsi inavyotakikana, akimtaka mwanakandarasi huyo kufanya kazi kwa utaratibu bila kuharakisha ili jengo hilo liwe sawa.

“Hakuna haja kuharakisha ujenzi wa jengo hili kisha hatimaye lilete madhara kwa watoto wetu. Jenga kwa njia inayofaa na kufuata utaratibu wa watalaamu wa ujenzi,” akashauri.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bi Elizabeth Nyangasi na mratibu wa masuala ya elimu katika Kanisa Katoliki Dayosisi ya Kitale, Padri Joseph Odongo, walisema ujenzi huo utakabili tatizo la ukosefu wa madarasa shuleni humo.

Mbunge wa Kwanza Ferdinand Wanyonyi akihutubia wanahabari baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa ghorofa ya madarasa manane katika Shule ya Upili ya Wasichana ya St Francis Assiss Kolongolo, Kwanza. PICHA | OSBORN MANYENGO