Habari Mseto

Wamatangi atikisa UDA kwa kufufua kauli ya “Mtu Mmoja, Kura Moja, Shilingi Moja”

May 13th, 2024 2 min read

KAMAU MAICHUHIE NA DAVID MCHUI

GAVANA wa Kiambu Kimani Wamatangi amefufua kampeni yake ya mtu-mmoja-kura-moja-shilingi moja, akitaka kaunti hiyo ipewe maeneo bunge sita zaidi kwa usawa katika ugawaji wa rasilimali na uwakilishi.

Katika kile kinachotarajiwa kuibua vita vya kisiasa vinavyowakutanisha viongozi katika maeneo yenye watu wengi katika kaunti hiyo kubwa, Gavana huyo amesema, wakati ujao wa kuangazia mipaka upya, atawasilisha kesi kali kwa tume ya uchaguzi, akitaka maeneo bunge yenye wakazi wengi kugawanywa.

Mkuu huyo wa Kaunti alibainisha kuwa Kiambu ina haki ya kuwa na maeneo ya ziada ya uchaguzi kwa uwakilishi wa haki katika Bunge la Kitaifa lenye idadi ya sasa ya takriban watu milioni tatu na baadhi ya maeneo bunge yenye zaidi ya watu 500,000.

Iwapo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itakubali pendekezo hilo, itaipatia kaunti zaidi ya Sh2 bilioni zaidi kila mwaka katika Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge na mgao wa maeneo bunge kwa ajili ya ujenzi wa barabara.

“Wakati wa msukosuko wa upambanuzi wa mipaka, tutasimama kidete kama kaunti ya Kiambu kwa sababu hakuna uhalali kwamba kuna maeneo bunge ambayo yanapokea pesa za CDF kwa takriban Sh140 milioni, ilhali wana chini ya robo ya idadi ya watu tuliyo nayo katika baadhi ya maeneo bunge ya Kiambu,” Bw Wamatangi alisema.

Mapitio ya mwisho ya kuangazia masuala ya mipaka yaliyounda maeneo bunge 290 yalifanywa Februari 2012 na Andrew Ligale-mwenyekiti wa Tume ya Muda Huru ya Mapitio ya Mipaka, huku kila eneo bunge likiwa na wastani wa watu 133,138. Kiwango cha idadi ya watu kilifikiwa baada ya kugawanya jumla ya watu, ambayo ilikuwa zaidi ya milioni 38 mnamo 2009.

Wakati huo huo, Baraza la Kitaifa la Makanisa nchini (NCCK) limeelezea wasiwasi wake kuhusu kucheleweshwa kwa kuwaajiri makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kongamano la NCCK kanda ya juu Mashariki lilisema kucheleweshwa kwa tume hiyo pia kumezuia mapitio ya mipaka ya uchaguzi.

Wakizungumza baada ya kongamano la wajumbe lililowaleta pamoja makasisi kutoka Meru, Tharaka Nithi, Isiolo na Marsabit, makasisi hao wameitaka serikali kuharakisha kushughulikia ucheleweshaji huo.

“Tunaona ni dhuluma kubwa kwamba nchi imekwenda kwa zaidi ya mwaka mmoja bila tume iliyoundwa ipasavyo kwa sababu ya makubaliano ya kisiasa. Tunamtaka Rais William Ruto na viongozi wengine wa kisiasa kuweka kando siasa,” mwenyekiti wa eneo hilo Rev Nicholas Nteere alisema.

Pia wanataka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutafuta ushauri kutoka kwa Mahakama Kuu kufuatia kutokamilika kwa makataa ya kikatiba ya mapitio ya mipaka.

Mchungaji Nteere pia alitoa wito wa kuwepo kwa mchakato unaoendeshwa na watu katika utekelezaji wa ripoti ya Mazungumzo ya Kitaifa ya pande mbili.

“Ripoti ya Nadco ilienda zaidi ya kushughulikia mzozo wa kisiasa na kupendekeza mabadiliko makubwa katika katiba na sheria za uchaguzi.

“Kutokana na athari ambayo mageuzi yanayopendekezwa yatakuwa nayo kwa maisha ya wananchi, tunaliomba Bunge kufanya mchakato huo uendeshwe na watu. Ripoti hiyo inapaswa kuwekwa wazi na Bunge lazima lijumuishe maoni ya umma,” makasisi hao walisema