Kimataifa

Watu 143 wafa Brazil kutokana na mafuriko

May 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MASHIRIKA

BRASILIA, BRAZIL

WATU 143 wameangamia nchini Brazil baada ya mvua kubwa kunyesha katika jimbo la Rio Grande do Sul kwa zaidi ya wiki mbili.

Mamlaka nchini Brazil imesema watu wengine 125 hawajulikani waliko katika jimbo hilo la kusini mwa Brazil huku viwango vya maji kwenye mito vikiripotiwa kupanda.

Idara ya hali ya hewa imesema mvua inayoendelea kunyesha “inatia wasiwasi”.

Mnamo Jumamosi, serikali ilitenga Sh315 bilioni ili kusaidia katika kukabiliana na janga hilo ambalo hadi sasa limewalazimisha watu 538,000 kuyahama makazi yao.

Mafuriko yaathiri wakazi wa Rio Grande do Sul nchini Brazil. Picha|Reuters

Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva amesema serikali kuu itajenga upya miundomsingi yote iliyoharibiwa na mvua katika jimbo hilo la Rio Grande do Sul.

“Tunafahamu kuwa si kila kitu kinaweza kurejeshwa, akina mama wamepoteza watoto wao na watoto wamepoteza mama zao,” alisema Lula kwenye mtandao wa kijamii wa X, katika taarifa yake ya kuadhimisha Siku ya akina Mama duniani.

Kwa upande wake, Rais Joe Biden wa Amerika amesema utawala wake utatuma msaada kwa waathiriwa wa mafuriko katika nchi hiyo.

“Tunatuma rambirambi zetu kwa wale waliopoteza jamaa zao nchini Brazil. Kando na hayo, tunawapongeza mashirika na watu binafsi waliojitolea kuwaokoa waathiriwa wa janga hilo. Tutatuma msaada nchini humo ili kuwasaidia waathiriwa,” Biden alisema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Mvua zaidi ilinyesha Jumapili na Jumatatu. Tangu mvua kuanza kunyesha katika nchi hiyo wiki mbili zilizopita, serikali inasema iko macho na kwamba inajaribu kupunguza athari ya mafuriko kwa kuhakikisha kuwa kiwango cha maji hakipandi katika Ziwa Guaiba, karibu na mji mkuu wa Porto Alegre.

Kando na kusababisha maafa, mafuriko hayo pia yameporomosha majengo na kusomba miundombinu.

Baadhi ya waathiriwa kwa sasa wanaishi shuleni, kambi za wakimbizi na wengine kupewa makazi ya muda serikali ikijaribi kutafuta suluhu ya kudumu.

Haya yanajiri huku mafuriko, radi na dhoruba yakiendelea kuhangaisha walimwengu mvua kubwa ikishuhudiwa katika nchi mbalimbali.

Wengi wamelazimika kuhama makazi yao kutafuta maeneo salama huku maelfu wakiendelea kupata matibabu.

Kwa sasa, nchi kadhaa zikiwemo China, Pakistan, Rwanda, Kenya, Tanzania, Italia, Slovenia na Ugiriki zinakabiliwa na mafuriko.

Japo idadi kamili ya vifo duniani haijabainishwa, inakadiriwa kuwa mafuriko hayo yamesababisha maafa ya maelfu ya watu.

Kwa mfano, zaidi ya watu 140 wamefariki dunia nchini Pakistan baada ya kupigwa na radi na matukio mengine yanayohusishwa na dhoruba huku taifa hilo likishuhudia mvua kubwa kuliko kawaida.