Hofu ya kipindupindu Ziwa Turkana likisomba vyoo vya hadhara hadi majumbani
SAMMY LUTTA NA LABAAN SHABAAN
ZIWA Turkana limejaa pomoni na kutapika maji mengi yaliyosomba uchafu kutoka msituni ambamo wakazi huenda kujisaidia hadharani.
Maeneo ambayo yako katika hatari ya kukumbwa na mlipuko wa kipindupindu ni Kalokol, Natirai, Longech na Kerio Delta.
Wakazi wengine wanakaa bila makao baada ya maji kuharibu makazi sehemu za Kang’atotha, Kataboi, Nachukui, Lowarengeak, na Todonyang. Kwa sasa wanaishi kwenye kibaridi cha usiku baada ya maji kutoka nje ya ziwa umbali wa mita mia moja.
Katika Kijiji cha Kalokol, mkazi Bw James Ekalale amesema maji yamemeza choo chake alichojenga karibu na ziwa.
Isitoshe, hata nyumba yake imesimama ndani ya maji. Bw Ekalale amebaki hoi sababu duka lake pia limejaa maji.
Hali hii isiyo ya kawaida katika eneo kame la Turkana imesababishwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa inayonyesha Ethiopia, Uganda na Kenya.
“Tuna hofu ya kuambukizwa magonjwa yanayosababishwa na maji machafu hususan kipundupindu,” alisema Bw Ekalale.
“Hatuwezi kumudu kujenga vyoo maeneo ya juu.”
Mkazi huyu amedokeza kuwa ni kawaida kwa vitongoji vya Longech, Kalokol, na Namukuse kukosa maji safi na pia kuna uhaba wa sehemu za kuendea haja.
Mwaka wa 2020, uongozi wa kaunti ya Turkana ulitoa ripoti ya visa 225 vya kipindupindu na mtu mmoja alifariki.
“Tunaomba tusaidiwe na dawa za kusafisha maji kwa sababu wakazi wengi wanategemea maji yasiyo salama kwa matumizi,” Bw Ekalale aliomba.
Serikali ya Kaunti ya Turkana imeshirikiana na asasi nyingine kusaidia wakazi walioathiriwa na ukame na mafuriko katika wadi za Kalokol na Kang’atotha, kaunti ndogo ya Turkana ya Kati.
Miongoni mwa mashirika yanayoshikana mkono na kaunti ni shirika la kustawisha ufugaji la Turkana Pastoralist Development Organization (TUPADO) na lile la kusaidia walemavu la CBM Global Disability Inclusion.
“Zaidi ya familia 3,000 zikiwemo zenye watu wanaoishi na ulemavu watanufaika. Tutasaidia walioathiriwa waimarishe maisha kupitia ufugaji wa mbuzi, kilimo, ufugaji wa kuku, uvuvi, na vyama vya maendeleo,” afisa mmoja wa CBM Global alisema.
Kwa moto uo huo, mkuu wa mipango ya TUPADO David Kang’ole amesema watahakikisha wanaganga athari za hali ya kiangazi iliyojiri mwaka jana.
“Tutaimarisha mshikamano wa kijamii kwa vijana, wanawake na wazee kwa kuwapa njia za kutega uchumi,” Bw Kang’ole aeleza.