Biashara, masomo yatatizika kufuatia daraja la Oldonyo Sabuk kuvunjika
NA LAWRENCE ONGARO
WAKAZI wa Oldonyo Sabuk, Kilimambogo, na Machakos wanaendelea kuwaza jinsi watakavyoendelea na biashara zao na shughuli nyingine za maisha baada ya daraja la Oldonyo Sabuk kukatika.
Kwa zaidi ya wiki tatu sasa, biashara zimeyumba kwa pande zote mbili za Kiambu na Machakos.
Wanafunzi nao wanahangaika.
Shule ambazo zilipata pigo la kukosa wanafunzi wengi siku ya ufunguzi ni Shule ya Msingi ya Oldonyo Sabuk na Shule ya Msingi ya Kilimambogo, Shule ya Upili ya St Mary, na chuo cha walimu cha Kilimambogo.
Jambo linalotia wakazi wa maeneo hayo wasiwasi ni kwamba, wasafiri wanaotumia boti kuvuka hadi ng’ambo ya pili huchukua muda wa dakika 30 kulingana na jinsi mawimbi ya Mto Athi yanavyovuma.
Aidha, wengi waliohojiwa walisema kuna hatari ya kuvuka kwa boti kwa sababu waendeshaji hawana ujuzi wa uzito wa watu na mizigo wanayobeba.
Mkazi mmoja wa Kilimambogo, Bw Charles Thuku, alisema kuwa Mto Athi unavuma kwa kasi na pia kuna viboko hatari majini.
“Hali ikisalia hivi kwa muda mrefu, bila shaka maisha ya wanafunzi na wafanyabiashara yatakuwa hatarini,” akasema Bw Thuku.
Alisema usafiri kwa kutumia magari kwa sasa ni ghali mno kwa sababu abiria wanalazimikia kuabiri magari ya kupitia Matuu hadi Githimani wakitoka Machakos kuelekea Kilimambogo.
Alisema mwendo huo kwa msafiri ni Sh1,000.
Bw Thuku alitoa wito kwa serikali kukarabati daraja hilo ili shughuli za kawaida zirejelewe.
Alisema siku ya soko kuu eneo la Kilimambogo huwa ni Jumapili na kila mfanyabiashara akiwa na mizigo mizito, analazimika kulipa ada ya hadi Sh2,000.
Baadhi ya bidhaa tofauti zinazovukishwa ni kuku, pombe, viazi, na maharagwe.
Alisema boti hizo ni chache na kwa hivyo watu wengi hufurika kila upande–wengine Kilimambogo na wengine Machakos–wakingoja kuziabiri.
Alisema wafanyakazi wengi wanaofanya kazi Del Monte na kuishi upande wa Machakos wamepata shida kubwa ya kufika kazini kila siku kutokana na changamoto hiyo.
Mhudumu wa bodaboda, Bw Joseph Musyoka, alisema kwa wiki tatu sasa, amesitisha biashara ya bodaboda kutokana na daraja hilo kubomoka.
“Sisi wanabodaboda tumepata pigo kubwa ajabu na hatuna njia nyingine ya kujikimu kimaisha,” aslisema Bw Musyoka.
Ifikapo jioni, watu wengi huonekana wakiharakisha shughuli zao ili usiku usiwapate kabla hawajavuka daraja hilo.