Limuru III: Gathoni Wamuchomba adai Mswada wa Fedha 2024 ni janga
NA MWANGI MUIRURI
MBUNGE wa Githunguri Bi Gathoni Wamuchomba amedai kwamba serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto imefanya maisha kuwa magumu kwa watu wa eneo la Mlima Kenya.
Akihutubu katika Kongamano la Limuru III mnamo Ijumaa, Bi Wamuchomba alidai serikali imefuta kazi watu 272 wa kutoka Mlimani.
Alidai kwamba licha ya kumpa Dkt Ruto asilimia 87 ya kura zao na kuunda serikali kwa asilimia 47, Naibu Rais Rigathi Gachagua ameshindwa kutetea watu wake.
Kuhusu Mswada wa Fedha wa 2024, alisema unaweka biashara nyingi katika hatari ya kuporomoka.
“Ukipitishwa kama ulivyo, basi biashara za Mlima Kenya zitaporomoka,” akasema Bi Wamuchomba, ambaye alijizolea nembo ya ‘Simba Jike’ kwa kutetea mwananchi wa kawaida almaarufu ‘Wanjiku’.
Pia alidai kwamba kwamba Mswada huo utatoza ushuru kahawa lakini miwa itaondolewa ushuru.
Alimsuta kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Bw Kimani Ichung’wah (Mbunge wa Kikuyu) kama “mtu wa kuramba huko pembeni kwa hao walio katika utawala na kukosa kuwafaa watu wa Mlima Kenya”.