Habari Mseto

Mbunge wa UDA aunga mkono walimu wa JSS kugoma

May 19th, 2024 1 min read

NA CHARLES WANYORO

MBUNGE wa Maara Kareke Mbiuki ameunga mkono mgomo wa walimu wa Sekondari ya Chini (Junior High) wanaopigania kuajiriwa rasmi, akiapa kutetea maslahi yao bungeni.

Mbunge huyo wa UDA amesema atapigania nyongeza ya mishahara kwa walimu wanagenzi wakati wenyeviti wa kamati mbalimbali za bunge watakapokutana na mwenzao wa Bajeti na Ugawaji rasilmali, Ndindi Nyoro Jumanne.

Akizungumza na makumi ya walimu hao wa JSS kutoka Maara, katika soko la Kieganguru, Bw Mbiuki aliwahimiza kuendelea kupaza sauti kuhusu masaibu yao akisema wengi wa wabunge wanaamini kilio chao ni cha haki.

“Hakuna mtu anapaswa kuwatishia eti mtafutwa kazi kwa sababu Katiba inasema kuandamana ni moja ya haki zenu. Tunawaunga mkono mia fil mia kwa sababu ni haki yenu kusukuma mfanyiwe haki,” akasema.

Bw Mbiuki alifichua kwamba wenyeviti wa kamati za bunge watakutana na Bw Nyoro wiki hii kupeana makadirio ya bajeti chini yao na kwamba wanaunga mkono malilio ya walimu.

“Maandamano yenu haya yamekuja wakati mzuri kwa sababu hiki ndio kipindi cha kuandaliwa kwa bajeti. Juzi tuliona mgomo wa wahudumu wa afya. Ingawa hawakupata kila kitu walichotaka, angalau hawakuondoka mikono mitupu,” akasema.