Kundi la kijamii Haiti laibuka likipinga vikali polisi wa Kenya kuhudumu nchini mwao
NA NYABOGA KIAGE
HUKU serikali ikilenga kuwatuma polisi kule Haiti mwezi huu, upinzani unaendelea kushuhudiwa kuhusu mpango huo ndani ya nchi hizo mbili.
Hakujakuwa na mawasiliano kutoka kwa viongozi saba ambao kwa sasa wanasimamia Haiti iwapo wapo tayari kushirikiana na polisi hao.
Vilevile viongozi wa magenge wameonya Kenya kutodhubutu kuwatuma wanajeshi wake katika taifa hilo.
Hapa nchini makundi ya kijamii na mawakili wanapambana mahakamani kuzuia polisi kutumwa nchi hiyo inayokabiliwa na misukosuko ya kisiasa.
Wikendi iliyopita kundi la Movement Unforgetable Dessalines Jean Jacques (MUDJJ) kutoka Haiti lilimshukuru wakili Ekuru Aukot kutokana na jitihada zake za kuwazuia polisi kutumwa Haiti.
Polisi kutoka Kenya wanatarajiwa kuwasili katika jiji kuu la Haiti Port au Prince kama sehemu ya maafisa wa usalama kutoka nchi mbalimbali wanaotarajiwa kurejesha utulivu Haiti.
Kwa mujibu wa MUDJJ, Bw Aukot amekuwa akitekeleza wajibu unaowaridhisha kwa kupinga kortini polisi kupelekwa Haiti.
“Tunakushukuru sana kutokana na juhudi ambazo umekuwa ukitekeleza kuzuia polisi kuletwa Haiti. Raia wa Haiti pia hawajakubaliana na hatua hiyo kwa kuwa ni kinyume cha katiba yao,” ikasema barua ya MUDJJ kwa Bw Aukot.
Walisema kuwa Kiongozi huyo wa Thirdway Alliance Party amechukua msimamo unaoana na ule wa raia wa Haiti na anastahili kuendelea kuwapigania katika korti za Kenya.
Kwa mujibu wa vuguvugu hilo, tatizo ambalo Haiti linakabiliwa nalo linaweza kutatuliwa tu na viongozi wa nchi hiyo wala si mataifa ya nje.
MUDJJ imeongeza kuwa nchi hiyo ambayo inapatikana ukanda Caribbean inakabiliwa na matatizo mengi ambayo yamesababishwa na kuingiliwa na mataifa ya nje yanayofumba ulimwengu macho kuwa yanawapa suluhu.
“Raia wa Haiti wanataka serikali ambayo itawawajibikia na kutimiza malengo yao. Si nchi za nje ambazo zitawaingilia na kuponda rasilimali zao kwa kudhibiti uchumi wao,” ikaongeza vuguvugu hilo.
Kwao, hatua ya Rais William Ruto inasukumwa na nchi za nje wala si umoja wa Afrika na nia yao ya kujiamulia mambo.
MUDJJ inasisitiza kuwa ajenda yao kuu ni kuhakikisha kuwa kuna amani Haiti na raia wanawachagua viongozi ambao wanawataka.
Tayari maafisa ambao ni sehemu ya jeshi la Marekani wapo Haiti wakijenga kambi kwa polisi kutoka Kenya.
Pia Bunge la Kitaifa na Baraza la Mawaziri limeidhinisha kutumwa kwa polisi 1,000 Haiti. Hata hivyo, hatua hiyo ilisimamishwa na korti ambayo iliitaja kama iliyokuwa ikikiuka katiba.
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry ambaye alikuwa akiunga kutumwa kwa polisi wa Kenya kule Haiti alilazimika kujiuzulu kutokana na ukosefu wa usalama.
Bw Henry kabla ya kujiuzulu alikuwa Kenya na hata akaandaa mazungumzo na Rais William Ruto japo alizuiwa kurejea nchini humo na makundi ya magenge.
Katika miezi mitatu ya kwanza ya 2024, zaidi ya watu 2,500 wamepoteza maisha yao kutokana na ghasia ambazo zinaendelea kushuhudiwa Haiti.
Afisa wa ngazi ya juu katika idara ya usalama jana alieleza Taifa Leo kuwa mkumbo wa kwanza wa polisi wa Kenya wataelekea Haiti wiki hii.
“Kila kitu kimekamilika na polisi 200 wataelekea Haiti wiki hii,” akasema afisa huyo ambaye hakutaka jina lake linukuliwe.
Polisi hao wataelekea Haiti wakati ambapo Rais William Ruto naye yuko ziarani Amerika, shughuli itakayochukua wiki moja.
Maafisa watakaotumwa Haiti watatoka idara mbalimbali ya polisi na inadaiwa ni wale ambao wamekuwa wakipambana na makundi ya kigaidi kama Al Shabaab na magenge mbalimbali.