Kimataifa

Rais wa Iran Ebrahim Raisi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni waangamia katika ajali ya helikopta

May 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

JANE SYOMBUA NA MASHIRIKA

RAIS wa Iran Ebrahim Raisi amethibitishwa kuaga dunia katika mkasa wa ndege ya helikopta katika mpaka wa Iran na Azerbaijan.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari nchini humo, watu tisa wanaaminika kuangamia akiwemo pia Waziri wa Mashauri ya Kigeni Hossein Amir Abdollahian, gavana wa jimbo hilo, imamu, walinzi, marubani na wafanyakazi wa ndege.

Tisa hao walikuwa wametoka hafla ya uzinduzi wa bwawa karibu na mpaka wa Azerbaijan na Iran, wakielekea jiji kuu la Tehran.

Duru zinaarifu kuwa ukungu mzito ndio ulichangia ajali hiyo iliyotokea mwendo wa saa nane mchana na kugubika taifa hilo la Mashariki ya Kati katika lindi la majonzi.

Mojawapo ya maswali yaliyoibuliwa ni sababu gani ndege hiyo iliruhusiwa kupaa ilhali hali ya anga ilikuwa mbaya. Msafara wa Bw Raisi ulikuwa kati ya helikopta zingine mbili zilizowabeba wajumbe zilizofanikiwa kutua vyema bila kukumbwa na hitilafu zozote lakini iliyombeba kiongozi wa nchi ikaanguka.

Iliwachukua waokoaji muda wa masaa 16 kufikia eneo la mkasa kutokana na msitu mkubwa na vijia visivyopitika.

Kifo cha Bw Raisi kimekuja wakati ambapo maandamano nchini Iran yamekuwa yakiendelea kutokea kifo cha kutatanisha cha mwanamke aliyepinga kuvalia kwa hijab kwa lazima nchini humo, Mahsa Amini, mnamo Septemba, 2022 na pia vita vya Israel dhidi ya mshirika mkuu wa Iran, Palestina.

Kiongozi mkuu nchini Iran, Ali Khamenei aliwasihi wananchi wa Iran wamkumbuke Bw Raisi kwenye maombi punde tu habari za mkasa ziliporipotiwa Jumapili.

“Mambo yote nchini yataendelea kama yalivyotarajiwa kabla ya mkasa. Hakuna chochote kitasitishwa,” Khamenei alihakikishia umma.

Habari kuhusu maombolezo ya kitaifa zitatangazwa huku mipango ya kumtafuta kiongozi mpya ikiendelea kwa mujibu wa sheria.

Kwa sasa, naibu rais wa kwanza, Mohammad Mokhber, atadhibiti mamlaka kwa kipindi cha mpito.

Kabla ya kifo chake, Raisi alionekana kuwa mrithi bora wa kiongozi mkuu, Ali Khamenei ambaye miaka yake inazidi kusonga na hali yake ya kiafya kuendelea kuzorota.

Hata kama Raisi alijulikana kama rais wa Iran, idhini zote zilipitia kwake Ali Khamenei, kama kiongozi mkuu.

Hiyo ilimaanisha Bw Raisi na wengineo walihudumu kulingana na amri ya Khamenei bila uhuru wa kujitegemea. Kabla ya kuwa rais, Raisi alikuwa na cheo cha ngazi za juu katika idara ya mahakama ambapo alisimamia kesi za haiba kubwa.