Serikali yachukua maelezo kimya kimya ya wakulima waliouziwa mbolea feki
WAKULIMA walionunua mbolea inayoshukiwa kuwa ghushi kutoka Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) wanaendelea kujitokeza na kuandikisha taarifa kwa polisi huku serikali ikikusanya data kimyakimya.
Wakulima kadhaa wamepiga ripoti katika vituo vya polisi kaunti ya Meru baada ya kugundua waliuziwa mbolea hiyo feki. Hata hivyo juhudi za kuthibitisha idadi ya wakulima waliopiga ripoti ziligonga mwamba kwa kuwa wakuu wa polisi walikataa kufichua wakisisitiza kuwa suala hilo linashughulikiwa Nairobi.
Mkuu wa polisi katika eneo la Imenti Kaskazini Ezekiel Chepkwony alitutuma kwa kamanda wa polisi wa kaunti na mkuu wa uchunguzi wa uhalifu ambao nao waliturejesha kwa makuu wa uchunguzi wa uhalifu katika kaunti ndogo.
Lakini Bi Stella Bundi, mkulima aliyenunua gunia la mbolea aina ya 10.26.10 NPK ambayo imeondolewa kutoka mabohari ya NCPB, alisema alipiga ripoti suala hilo katika kituo cha polisi cha Meru na depo la NCPB katika kaunti hiyo. Bi Bundi alisema alinunua mbolea hiyo ya ruzuku mnamo Machi 21 lakini akagundua ilikuwa feki alipokuwa akiitumia kwa upanzi.
“Wafanyakazi wangu waligundua kwamba mbolea hiyo ya NPK ilikuwa na kinyesi cha ng’ombe na wakanifahamisha. Nimepeleka sampuli kwa NCPB na katika kituo cha polisi ambako nilipata nambari ya kuripoti. Nimefahamishwa kwamba serikali inakusanya data za wakulima waliopokea mbolea hiyo ili walipwe fidia,” alisema.
Bw Jacob Mbaya, mkulima kutoka Uku, Imenti Kusini pia amepata hasara baada ya kununua magunia sita ya mbolea aina ya Nafaka NPK kutoka depo la NCPB kaunti ya Meru.
Wafanyakazi wangu walinifahamisha kuwa mbolea ilikuwa na vipande vya mawe. Niliwashauri wajaribu kuiweka kwa maji na kuthibitisha hofu yao. Nimepoteza Sh15,000 na msimu wa upanzi umepita,” alisema Bw Mbaya.
Hata hivyo, alisema kwamba wakulima ambao walilaghaiwa, watalipwa fidia.
Haya yanajiri huku waziri huyo akiendelea kushutumiwa kwa kukanusha kuwepo kwa mbolea feki nchini.
Mbunge wa Mbeere Kaskazini Geoffrey Ruku amemkosoa vikali Bw Linturi na kumtaka kuwajibika kikamilifu sakata hiyo ambayo imeacha wakulima wakiteseka.