Habari Mseto

Mateso mpaka lini? Sh2.4 bilioni zakosa kuridhisha madaktari kufuta mgomo

April 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ANGELA OKETCH na RICHARD MUNGUTI

WAKENYA wataendelea kuteseka kwa muda usiojulikana huku madaktari wakishikilia msimamo wao mkali wa kuendelea na mgomo licha ya serikali kuahidi kutimiza baadhi ya matakwa yao.

Huku madaktari wakikaa ngumu, maafisa wa utabibu wamegoma, wanafamasia na wataalamu wa maabara nao pia wanatishia kugoma iwapo matakwa yao kuhusu mishahara na mazingira ya kazi hayatatimizwa.

Hii itasababisha huduma za afya kukwama kabisa kote nchini na kusababishia Wakenya mahangaiko tele.

Mgomo wa madaktari kote nchini sasa umeingia siku ya 23 Alhamisi, huku wagonjwa wanaosaka huduma za afya katika vituo vya afya mbalimbali vya umma wakizidi kuteseka.

Jumatano, Mahakama ya Leba iliagiza madaktari kusitisha mgomo huo huku Jaji Byram Ongaya akiamuru mazungumzo hayo kukamilika katika muda wa siku 14 ambapo pande husika zitarejea kortini Aprili 17.

Vile vile, aliagiza Baraza la Magavana kukusanya na kuwasilisha kortini ripoti kuhusu uhaba wa wahudumu wa afya katika hospitali za kaunti zao.

Hata hivyo, madaktari wamesisitiza kwamba, hawatarejea kazini hadi serikali na magavana watakaposuluhisha malalamishi yao.

Kupitia chama chao cha Muungano wa Madaktari na Wataalamu wa Meno (KMPDU), walipuuzilia mbali tangazo lililotolewa na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Felix Koskei, kuwa serikali imeachilia Sh2.4 bilioni za madaktari wanagenzi kuajiriwa.

“Kwa upande wa serikali kuu, hatua zifuatazo zimechukuliwa ili kutimiza majukumu yake: imewezesha malipo ya malimbikizi ya mishahara yanayodaiwa serikali kuu kutokana na makubaliano ya pamoja ( CBA) 2017-2021,” alisema.

“Serikali imepata bajeti iliyohitajika ya Sh2.4 bilioni ili kufanikisha mchakato wa kuajiri kundi la mwaka wa 2023/24 la madaktari kuambatana na masharti yaliyotolewa na Tume ya Malipo ya Mishahara (SRC).”

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Muungano wa Madaktari Nchini (KMPDU), Dkt Davji Atellah, alisema pesa zilizodaiwa kutolewa na serikali zilidhamiriwa wahudumu wote wa sekta ya afya na sio madaktari pekee.

“Hii ni hujuma kuu, hauwezi kudai umeachilia Sh2.4 bilioni kwa madaktari wanagenzi ilhali umepunguza mishahara yao kwa asilimia 91. Ni dharau tupu. Hatutaruhusu hili,” alisema Dkt Davji.

“Ili walipwe kuambatana na SRC, inamaanisha wameenda kinyume na agizo lililotolewa na mahakama 2017 kuhusu utekelezaji wa CBA.

Wamekaidi amri ya korti. Bajeti ya kuwalipa madaktari wote wanagenzi ilikuwa Sh4.8 bilioni na wamepunguza mishahara kwa nusu,” alisema Dkt Atella.

KMPDU imelalamikia hali ya Wizara ya Afya na Baraza la Magavana kukataa kuwapa madaktari ajira ya kudumu.

“Magavana hawatulipi kwa kutumia hela zao. Wamekuwa wakisisitiza kwamba, wao ni waajiri wetu wakati hata hawawezi kutulipa mishahara. Uangalizi unaweza kuwekwa chini ya kaunti lakini michakato ya kupandishwa cheo na bima za afya kunapaswa kuwa katika huduma ya umma,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa KMPDU, Dkt Dennis Miskellah.

Wakati huo huo, Waziri wa Afya Susan Nakhumicha anakabiliwa na tishio la kutimuliwa ofisini ikiwa Bunge la Kitaifa litapitisha hoja inayolenga kumng’atua kwa msingi wa usimamizi mbaya wa sekta ya afya.

Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, kupitia hoja iliyowasilishwa kwa Karani wa Bunge la Kitaifa, Samuel Njoroge, anataka Bi Nakhumicha abanduliwe afisini kwa ukiukaji wa katiba na kushindwa kufanya kazi.

“Kutokana na mgomo wa madaktari, haki ya Wakenya wengi kuhusu kuishi pamoja na haki ya kupata huduma ya afya ya zimekiukwa tangu mgomo huo ulipoanza mwezi uliopita,” alisema Bw Owino.