Mama aacha mtoto hospitalini na kutoroka baada ya bili ya Sh23,000 kumlemea
MWANAMKE mmoja mwenye umri wa miaka 21 katika Kaunti ya Nakuru aliacha mtoto wake hospitalini na kutoroka baada ya kushindwa kulipa bili ya Sh23,000.
Bi Mary Wangui alilazwa katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya Nakuru mnamo Machi 11, alikofanyiwa upasuaji.
“Nilikuwa na mimba ya mwezi mmoja na nililazimika kwenda hospitalini na binti yangu kwa sababu hakukuwa na mtu wa kuachwa naye nyumbani. Jioni niliyolazwa, baba yake alirudi naye nyumbani lakini alilia usiku wote na akalazimika kumrudisha asubuhi na hivyo ndivyo niliishi na binti yangu hospitalini,” alisimulia.
Baada ya upasuaji kufaulu, Bi Wangui alilazwa katika wodi kwa wiki tatu apate afueni. Licha ya familia kufurahia kupona kwake, ililemewa na mzigo wa bili ya Sh23,000, kiasi ambacho hakuwa na uwezo wa kukilipa.
Familia ilijaribu kutafuta usaidizi kutoka kwa marafiki na familia lakini haikuweza kupata pesa za kulipa bili ambayo ilikuwa ikiongezeka, na ndipo Bi Wangui alifanya uamuzi wa kuacha mtoto wake mwenye umri wa miezi tisa hospitalini.
Alitoroka saa saba wagonjwa walipokuwa wametembelewa na jamaa zao na kusaidiwa na marafiki kufika nyumbani. Mumewe, ambaye alikuwa amekosa pesa za kulipa bili alishangaa kumuona.
Bi Wangui aliambia Taifa Leo katika mahojiano kwamba alifanya uamuzi huo baada ya kilio chake kwa wafanyakazi wa kijamii katika hospitali hiyo ya umma kukataliwa.
Hali yao ya kifedha ilizidi kuwa mbaya wakashindwa kulipa kodi ya nyumba ambayo wanadaiwa malimbikizi ya miezi minne. Mapato ya mumewe anayechuuza ndizi yamepungua.
“Niliomba wafanyakazi wa kijamii wanisaidie kuzungumza na usimamizi upunguze bili au kuifuta lakini wakaniambia haiwezekani. Hatuna pesa, mume wangu ni mchuuzi na anachopata kwa kuuza ndizi hakitoshi,” alisema.
Mtoto huyo alipelekwa katika makao ya watoto hadi bili itakapolipwa huku familia ikiwa imetamauka.
Kisa hicho kiliripotiwa katika kituo kidogo cha polisi kilicho uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Nakuru.
Dkt James Waweru, msimamizi wa hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nakuru, alisema hospitali ilichukua hatua zinazofaa kulinda maslahi ya mtoto huyo na kwamba kisa hicho sasa kiko mikononi mwa idara ya watoto.